Oct 21, 2020 13:26 UTC
  • Rouhani: Kuhitimishwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran ni ushindi wa mantiki ya akili dhidi ya mabavu

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuhitimishwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran ni ushindi wa mantiki ya akili na ukweli dhidi ya utumiaji mabavu.

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo katika kikao na baraza lake la mawaziri mjini Tehran ambapo ameashiria kumalizika muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran na kusema: "Kwa miaka kadhaa sasa Marekani imekuwa ikijaribu kulinyima taifa la Iran haki zake lakini imeshindwa na haijaweza kufikia malengo yake."

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia kushindwa utawala wa Kizayuni wa Israel katika kushawishi nchi zilizoafiki mapatano ya nyuklia ya JCPOA kujiondoa katika mapatano hayo. Ameongeza kuwa, Marekani imetengwa katika njama zake za kutaka vikwazo vya silaha dhidi ya Iran virefushwe. Amesema Marekani imepuuzwa hata na waitifaki wake katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

 

Rouhani amesema Iran ilitumia busara na tadibiri baada ya Marekani kujiondoa katika JCPOA ambapo ilichukua hatua ya kisheria ya kupunguza uwajibikaji wake katika mapatano hayo ya nyuklia. Amesema hatua hiyo ya Iran ilichukuliwa kwa busara na umakini ambapo maadui na marafiki wameshindwa kuikosoa Tehran.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema pia kuwa, sera za Marekani kuhusu Iran si sahihi hata kidogo na amesisitiza kwamba, suala la nani au chama gani kitashinda katika uchaguzi wa rais nchini Marekani si muhimu kwa Iran, kwa sababu atakayeshinda hatakuwa na budi ila kusalimu amri mbele ya taifa la Iran, na hakuna chaguo au njia nyingine ghairi ya hiyo.

Tags