Oct 22, 2020 02:36 UTC
  • Mazoezi ya Kijeshi ya Walinzi wa Anga ya Velayat-99; kujitayarisha kwa ajili ya kukabiliana na vitisho

Moja kati ya malengo ya kistratijia ya mafundisho ya kijeshi ya Iran ni kulinda utayarifu na kuimarisha uwezo wa jeshi kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Katika mkondo huo mazoezi ya kitaalamu ya Jeshi la Anga yaliyopewa jina la Walinzi wa Anga ya Velayat-99 yalianza jana Jumatano yakiongozwa na kusimamiwa na kambi kubwa ya Jeshi la Anga la Iran. Lengo la mazoezi hayo limetajwa kuwa ni kunyanua juu uwezo na utayarifu wa jeshi la Iran kwa kushirikisha vikosi vya Jeshi la Anga na kikosi cha anga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (Sepah) katika mazingira yanayokaribiana sana na ya vita halisi. Mazoezi hayo yanafanyika katika eneo lenye ukubwa wa zaidi ya nusu ya ardhi ya Iran.

Brigedia Jenerali Qader Rahimzadeh ambaye ni kamanda wa mazoezi ya Jeshi la Anga ya Walinzi wa Anga ya Vilayat-99 ameashiria utumiaji wa aina mbalimbali za ndege za kuwinda, kurusha mabomu na makombora, ndege zisizo na rubani na kadhalika katika mazoezi hayo na kusema kuwa, kwa mara ya kwanza kabisa katika mazoezi haya kunatumiwa kwa asilimia mia moja kizazi kipya cha zana na silaha za kijeshi zilizotengezwa na watalaamu wa ndani ya nchi.

Makamanda wa jeshi la Iran

Mazoezi makubwa na ya kitaalamu ya jeshi ni ishara ya uwezo wa kijeshi katika upeo wa kistratijia na jambo lenye umuhimu mkubwa katika pande kadhaa. Kwanza mazoezi hayo yanaonyesha uwezo wa kujilinda na kujihami mkabala wa vitisho, na vilevile uwezo wa kukabiliana na uchokozi na hujuma yoyote ya adui.

Suala la pili lenye umuhimu mkubwa katika kufanya maoezi kama haya ni kutegemea utaalamu wa wasomi wa ndani ya nchi katika kudhamini mahitaji ya kiulinzi. Haya yote kwa hakika ni jibu mwafaka kwa vikwazo haramu vya Marekani dhidi ya Iran.

Katika mojawapo ya hotuba zake, Amiri Jeshi wa majeshi yote ya Iran, Ayatullah Ali Khamenei aliashiria sifa kuu ya nguvu za taifa la Iran na kusisitiza kuwa, lengo la sera za kujilinda za Jamhuri ya Kiislamu ni kuzuia hujuma ya aina yoyote ya mabeberu wa kimataifa. Alisema: Maadui wanapaswa kuelewa kuwa, iwapo watafikiria kuishambulia ardhi ya Iran watakabiliana na jibu kali; kwa sababu inawezekana wao wakawa waanzilishi wa vita lakini hapana shaka kuwa hawataweza kumaliza vita hivyo.

Ayarullah Ali Khamenei

Hii leo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uwezo mkubwa katika masuala ya anga, makombora na uwezo wa jeshi la baharini na nchi kavu. Hata hivyo uwezo huo si tishio kwa usalama na amani ya kanda hii ya Magharibi mwa Asia; na tofauti na madai ya maadui na madola ya kibeberu, siasa za Iran kuhusu eneo hilo zimejengeka kwa msingi wa kujiepusha na vita na machafuko, na kulingania ushirikiano katika masuala ya kulinda usalama. Kwa sababu hiyo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ametoa pendekezo la amani shirikishi la "Amani ya Hormuz" kwa viongozi wa nchi za kandokando ya Ghuba ya Uajemi na kuwataka wautajirishe zaidi mpango huo na kushiriki katika utekelezaji wake. 

Vilevile katika hotuba yake ya Jumanne ya wiki hii katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichochunguza hali ya eneo la Ghuba ya Uajemi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Muhammad Javad Zarif aliikosoa Marekani kama muuzaji mkubwa zaidi wa silaha katika eneo hilo na kusema: "Yumkini nchi ikanunua silaha tata zaidi duniani lakini ukweli ni kwamba, usalama na amani ni vitu ambavyo havinunuliwi kwa pesa."
Zarif ameeleza mtazamo wa Iran kuhusu usalama wa Ghuba ya Uajemi na kusema: "Kunahitajika ushirikiano wa nchi zote za eneo hili kwa ajili ya kuanzisha mazungumzo ya pande zote na kuimarisha usalama wa kanda nzima; la sivyo vizazi vijavyo vitakabiliwa na vita na machafuko."