Oct 22, 2020 07:59 UTC
  • Zarif: Eneo la Ghuba ya Uajemi lichague ama amani au ukosefu wa uthabiti

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema eneo la Ghuba ya Uajemi sharti likhitari moja kati ya mambo mawili, ama amani au ukosefu wa uthabiti.

Muhammad Javad Zarif amesema hayo katika ujumbe wake wa Twitter alioutuma jana Jumatano kwa lugha ya Kiarabu, ambapo ameashiria sehemu ya hotuba yake aliyoitoa katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliofanyika kwa njia ya intaneti, juu ya hali ya Ghuba ya Uajemi.

Zarif amesema: Tunaweza kuchagua kubakia mateka wa yaliyopita, na taharuki na ukosefu wa usalama uendelee kushuhudiwa, au tuchague maisha ya amani, usalama, ustawi na mafanikio kwa wote. Tutakachochagua inapasa kiwe wazi kabisa kwa kila mmoja.

Mkutano huo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ulioitishwa na Russia ambaye ni rais wa mzunguko wa taasisi hiyo kubwa zaidi ya UN ulifanyika Jumanne katika ngazi ya Mawaziri wa Mambo ya Nje, ambapo Dakta Zarif alihutubia pia.

Trump na Mfalme Salman wakisaini makubaliano ya mauzo ya silaha zenye thamani ya mabilioni ya dola

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria kuhusu pendekezo la Iran la kuimarisha amani katika eneo lililopewa jina la "Muungano wa Matumaini" au "Amani ya Hormuz" (HOPE) na kusisitiza kuwa, Marekani ndio muuzaji mkubwa zaidi wa silaha katika eneo la Asia Magharibi.

Dakta Zarif ameonya dhidi ya machaguo ghalati kama vile kununua usalama kutoka kwa wengine, kutafuta usalama kwa madhara ya ukosefu wa usalama kwa majirani, na mashindano ya ubabe, akisisitiza kuwa, yote haya yamekuwa na matokeo mabaya.

 

Tags

Maoni