Oct 24, 2020 07:49 UTC
  • Iran yamuwekea vikwazo balozi wa Marekani nchini Iraq kwa ugaidi

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemuwekea vikwazo Balozi wa Marekani nchini Iraq, Matthew Tueller kwa kujihusisha na vitendo vya kigaidi.

Taarifa ya jana Ijumaa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema Jamhuri ya Kiislamu imemuweka Tueller pamoja na wanadiplomasia wengine wawili wa Marekani katika orodha nyeusi, kutokana na wao kujihusisha na vitendo vya ugaidi, kukanyaga haki za msingi za binadamu na kuliwekea taifa la Iran vikwazo vya kikatili na vilivyo kinyume cha sheria.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Tueller pamoja na Naibu Balozi wa Marekani mjini Baghdad, Steve Fagin, na mkuu wa ubalozi mdogo wa US katika eneo la Erbil, Rob Waller wamewekewa vikwazo hivyo kwa mujibu wa sheria iliyopasishwa mwaka 2017 na Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa lengo la kukabiliana na harakati za ugaidi za Marekani katika eneo la Asia Magharibi.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeeleza bayana katika taarifa hiyo kuwa, wanadiplomasia hao watatu wa Marekani wamehusika moja kwa moja katika kupanga, kufadhili, kuongoza na kutekeleza vitendo vya ugaidi dhidi ya maslahi ya serikali na taifa la Iran.

Mashahidi Qassem Soleimani na Abu Mahdi al-Muhandis

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, mbali na maafisa hao wa kibalozi wa Marekani kuyaunga mkono kwa hali na mali makundi ya kigaidi katika eneo kama Daesh na Jabhat al-Nusra, lakini walihusika pia na mauaji ya kigaidi ya Haji Qassem Soleimani.

Itakumbukwa kuwa, Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na Abu Mahdi al-Muhandis, Naibu Kamanda wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq (Hashd al Shaabi) pamoja na wanamapambano wengine kadhaa waliuawa shahidi mapema mwaka huu katika shambulizi la kigaidi la jeshi la Marekani katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

 

Tags

Maoni