Oct 26, 2020 11:36 UTC
  • Shamkhani: Kauli za Macron dhidi ya Uislamu zinaonyesha ni mwanagenzi wa siasa

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema matamshi ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu yanayotolewa na Rais Emmanuel Macron yamedhihirisha uanagenzi wa kisiasa alionao kiongozi huyo wa Ufaransa.

Ali Shamkhani amesema hayo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kubainisha kuwa, mienendo ya Macron isiyo na mantiki tena hadharani dhidi ya Uislamu inaonyesha namna alivyo mwanagenzi katika siasa.

Shamkhani amemtaka Macron aisome historia kwa makini na kwa kina badala ya kujiunga na mkumbo uliofeli wa Marekani na Uzayuni ambao daima unaupiga vita Uislamu.

Afisa huyo wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, matamshi machafu ya Macron dhidi ya Uislamu hayakubaliki na yanaenda kinyume na ustaarabu, muruwa na utamaduni wa jamii ya wanadamu.

Baada ya kudai mapema mwezi huu kuwa Uislamu ni dini ambayo ipo katika mgogoro mkubwa kote duniani, Jumatano iliyopita Macron alisema Ufaransa katu haitalaani vibonzo vya kumvunjia heshima Mtume Muhammad (SAW).

Maandamano dhidi ya Macron na misimamo yake dhidi ya Uislamu na Waislamu

Aidha ametishia kuwafukuza mamia ya Waislamun nchini humo, kwa kisingizio cha kukabiliana na kile kinachotajwa kuwa misimamo mikali ya kufurutu ada.

Viongozi mbalimbali wa ulimwengu wa Kiislamu wakiwemo wa Kuwait, Uturuki, Iran, na Morocco wameshatoa taarifa za kulaani chokochoko hizi mpya za Macron.

Tags

Maoni