Oct 27, 2020 02:29 UTC
  • Iran: Marekani ikithubutu kuanzisha vita, haitakuwa na uwezo wa kuvimaliza

Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kama Wamarekani wataanzisha vita basi wamalizaji wa vita hivyo hawatakuwa wao.

Brigedia Jenerali Muhammad Bagheri amesisitiza kuwa, ndio maana vita vya kijeshi vya Marekani hii leo vimekuwa ni vya niaba ikihofia kuacha athari.

Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria uwezo wa kiulinzi wa Iran, nguvu za kumfanya adui asithubutu kushambulia na mshikamano wa vikosi vya ulinzi vya taifa hili na kusema kuwa, vikosi vya ulinzi vya Iran vipo katika hali na mazingira bora kabisa hii leo.

Brigedia Jenerali Bagheri ameashiria hatua ya Marekani ya kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kuwawekea wananchi wa Iran vikwazo vya kidhalimu na akaeleza kwamba, walimwengu wote wamekiri kwamba, Iran imefungamana na ahadi zake, lakini pamoja na hayo na licha ya Washington yenyewe kukiuka makubaliano hayo imewawekea vikwazo vya kidhulma wananchi wa taifa hili.

Dhulfikar moja ya makombora ya Iran

 

Aidha amesema, lengo la adui dhidi ya Iran liko wazi kabisa nalo si jingine bali ni kuifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran isalimu amri na kufuata amri na matakwa ya kibabe ya utawala wa Marekani.

Ikumbukwe kuwa, viongozi mbalimbali wa Jamhuri ya Kiislamuu ya Iran wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kwamba, katu taifa hili la Kiislamu haliko tayari kusalimu amri mbele ya matakwa haramu ya Marekani na limesimama kidete katika njia hii.