Oct 28, 2020 07:52 UTC
  • Ayatullah Larijani ataka Waislamu waungane kukabili chuki dhidi yao

Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Iran amelaani vikali hatua ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ya kuunga mkono kitendo cha kifidhuli cha jarida la Charlie Hebdo cha kuchapisha tena vibonzo vya kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW na kusisitiza kuwa, kuna udharura wa Waislamu kuwa na umoja na ushirikiano katika kukabiliana na chuki dhidi yao na Uislamu.

Ayatullah Sadiq Amoli Larijani amebainisha kuwa, "matusi haya yasiyo na mantiki, ya kejeli na udhalilishaji yaliyochapishwa na jarida la Kifaransa, na vile vile uungaji mkono usio na maana na usio halalishika wa Macron kwa vitendo hivyo vya kufuru ada hauwezi kuhalalishwa kwa hali yoyote ile."

Ameeleza bayana kuwa, kuna Waislamu bilioni mbili kote duniani wanaoweza kusimama kidete kupinga chokochoko hizo za Ufaransa za kumvunjia heshima Mtume wa Uislamu, Muhammad SAW.

Ayatullah Larijani amebainisha kuwa: Watu mfano wa Macron wanapaswa kuelewa kuwa hawawezi kusimamisha nuru ya kuenea Uislamu kwa vitendo vyao vya kipumbavu, visivyo na mantiki wala murua.

Maandamano ya kulaani kitendo cha kifidhuli cha jarida la Kifaransa la Charlie Hebdo cha kuchapisha tena vibonzo vya kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW

Kadhalika Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Iran amesisitiza kuwa, Waislamu wote wanapaswa kusimama na kupaza sauti moja ya kulaani na kupinga vitendo vya kihaini vya kuvunjiwa heshima Mtume Mtukufu wa Uislamu ambaye anapendwa na kuenziwa na hata wasiokuwa Waislamu.

Amemhutu Rais wa Ufaransa kwa kumuambia kuwa, anapaswa kufahamu kwamba jibu la Ulimwengu wa Kiislamu kwa vitendo hivyo vya kijahili halitakuwa jepesi. 

Tags