Oct 28, 2020 12:26 UTC
  • Rais Rouhani: Wamagharibi wasijiingize kwenye masuala ya ndani ya Waislamu

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, kama nchi za Magharibi, za Ulaya na Ufaransa ni wakweli katika madai yao kwamba zinapigania amani, udugu, usalama na utulivu katika jamii ya mwanadamu basi zinapaswa kuacha kuingilia masuala ya ndani ya Waislamu.

Rais Hassan Rouhani amesema hayo leo Jumatano katika kikao cha Baraza la Mawaziri la serikali yake na kuongeza kuwa, kumvunjia heshima Mtume wa Mwenyezi Mungu ni utovu wa maadili, ni kuchochea machafuko na ni kujeruhi hisia za mabilioni ya Waislamu na wasio Waislamu. Wale waliongia kwenye njia hiyo ghalati wanapaswa kufanya haraka kurekebisha makosa yao na waingie katika njia ya uadilifu, maadili na kuheshimu itikadi za dini zote za Mwenyezi Mungu.

Rais Rouhani ameongeza kuwa, Mtume Muhammad SAW ni mwalimu wa wanadamu wote na ni rehema kwa viumbe wote. Inashangaza kuona watu wanaodai wamestaarabika na ni viranja wa demokrasia, wanawachokoza watu wengine bila sababu na wanachochea machafuko na umwagaji wa damu.

Na hatukukutuma (Ewe Muhammad) ila uwe rehema kwa walimwengu wote

 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, kila mtu wa Ulaya na wote wanaoishi Mashariki na Magharibi wana deni kwa Mtume Muhammad SAW, Yeye ni mwalimu wa wanadamu wote. Inashangaza kuona nchi zinazodai zina uhuru, zinaheshimu haki na sheria, zinachochea kuvunjiwa heshima matukufu ya watu wengine, matukufu ambayo watu hao wanayatukuza kwa dhati yao yote.

Vilevile Rais Rouhani ameelezea kufurahishwa kwake na jinsi ulimwengu wa Kiislamu ulivyosimama kidete kutetea matukufu yake na kuwaeleza viongozi wa nchi za Magharibi kwamba, radiamali hii ya Waislamu ambayo imeoneshwa kwa wakati mwafaka na bila ya kuchelewa ni ushahidi madhubuti kwamba daima ulimwengu wa Kiislamu utaendelea kumpenda kwa dhati kiongozi wao mkuu, Bwana Mtume Muhammad SAW.

Tags

Maoni