Oct 29, 2020 02:28 UTC
  • Mkuu wa shirika la utangazaji la Iran IRIB asisitiza kuvishtaki vyombo vya habari vinavyoeneza uhasama na chuki dhidi ya Iran

Karibu kanali 130 zinazotangaza kwa lugha ya Kifarsi na nyingine karibu 140 zinazotangaza kwa lugha na lahaja tofauti za Kiirani zinatangaza vipindi vyenye chuki dhidi ya Iran na kulenga moja kwa moja utamaduni na utambulisho wa Kiirani na Kiislamu wa taifa hili.

Hujuma hiyo ina taathira kubwa na tofauti ambazo zina umuhimu wa kufuatiliwa kisheria. Abdulali Ali Askari, Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Redio na Televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelizungumzia suala hilo katika kikao cha kwanza kilichofanyika hivi karibuni cha Baraza la Utaalamu na Stratijia la Masuala ya Kisheria la IRIBI .

Kwa kutilia maanani nafasi muhimu ya shirika la IRIB na udharura wa kunufaika na mfumo wa sheria katika kukabiliana na kanali za satalaiti zinazotangaza matangazo yenye chuki na uhasama dhidi ya mfumo wa Kislamu wa Iran, suala hilo linaweza kuchunguzwa katika mitazamo miwili.

Mtazamo wa kwanza ni kufuatiliwa jambo hilo katika mkondo wa sheria na mikataba ya kimataifa inayohusiana na masuala ya utangazaji. Katika uwanja huo, kuna masuala muhimu ambayo yanapaswa kuzingatiwa kwa makini na kisheria licha ya maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika sekta ya utangazaji na vyombo vya habari.

Shirika la IRIB

Mtazamo wa pili ni kukabiliana  moja kwa moja na pande pamoja na watu waovu wanaochochewa na vyombo hivyo vya habari vya nchi za kigeni kwa ajili ya kutilia shaka ukweli wa habari na vipindi vinavyotangazwa na shirika la IRIB. Upotoshaji wa makusudi wa habari zinazotangazwa na chombo hiki cha habari ambacho kina mchango mkubwa katika marekebisho na uongozaji wa fikra za jamii, bila shaka ni njama inayotekelezwa na watu walio na uelewa na wanaofuatiliwa malengo maalumu ya kistratijia katika nyanya za upashaji habari kwa madhumuni ya kuchochea machafuko ya ndani. Jambo hili linatekelezwa hasa na watu na wanaharakati maalumu wanaoshughulikia mambo tofauti katika mitandao ya kijamii, vyombo vya habari na kanali za satalaiti.

Kuhusu kadhia hiyo, baadhi ya wataalamu wa vyombo vya habari wanasema kuwa waharibifu hao ambao wanataka kuuangusha mfumo wa Kiiislamu tokea ndani wamebadilisha mbinu zao za uhaini na usaliti na sasa wanatumia njia laini zisizohisika kirahisi kufikia malengo yao hayo ya kiusaliti.

Andrew Korybko, mwandishi na mchambuzi wa masuala ya kisiasa anaashiria katika kitabu chake kinachohusiana na masuala ya vita laini, uchaguzi uliofanyika nchini Iran mwaka 2009 na kuandika: Baada ya uzoefu mchungu uliogharimu pesa nyingi wa vita vya Iraq na hatimaye kupelekea kutekwa nchi hiyo mwaka 2003, Marekani iliamua kuendesha vita laini badala ya kutumia silaha za kawaida. Hii ni kwa sababu ilipata funzo muhimu kwamba badala ya kuendesha vita vya silaha ni bora kuwatumia vibaraka wa ndani kufikia malengo yake katika mataifa tofauti. Kwa ibara nyingine ni kuwa Marekani iliamua kuachana pakubwa na vita vya kawaida na badala yake kutumia vita vya niaba kulinda maslahi yake. Vita hivyo kwa hakika ni vita visivyo na uwiano, vya ndani na kiraia ambavyo kwa kawaida majeshi na vyombo vya usalama huwa havina uwezo wa kukabiliana navyo.

Andrew Korybko

Kimsingi katika zama hizi Marekani hutumia vyombo vya propaganda na habari na vilevile kanali za satalaiti katika kupanga njama za vita laini dhidi ya nchi na mataifa mbalimbali. Mwaka uliopita pia na kufuatia machafuko yaliyoibuliwa katika baadhi ya miji ya Iran kufuatia uamuzi wa kutekelezwa sheria ya kudhibiti matumizi ya mafuta, kanali za satalaiti zinazofungamana na Marekai, bila kupoteza wakati, ziliingia kwenye medani ya fitina na uchochezi dhidi ya Iran na kuunga mkono moja kwa moja machafuko hayo. Hatua hiyo inathibitisha wazi kwamba kanali za satalaiti na mitandao ya kijamii inachukuliwa na nchi za kibeberu kuwa vyombo vizuri vinavyoweza kutumika kuendeshea vita laini dhidi ya serikali huru zinazopinga siasa za mabavu na za kikoloni za nchi hizo. Ni kwa kuzingatia nukta hiyo muhimu ndipo mkuu wa shirika la utangazaji la IRIB akasisitiza udharura wa kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi ya uchochezi unaofanywa na kanali za satalaiti zinazodhaminiwa kwa hali na mali na nchi za Magharibi kwa lengo la kuchafua na kuharibu fikra za jamii ya Iran.

Maoni