Oct 29, 2020 12:10 UTC
  • Mkutano wa 34 wa kimataifa wa Umoja wa Kiislamu waanza mjini Tehran

Mkutano wa 34 wa kimataifa wa Umoja wa Kiislamu umeanza kufanyika mjini Tehran ukihudhuriwa na shakhsia 167 wa ulimwengu wa Kiislamu.

Kongamano hilo lililoanza leo linatarajiwa kuendelea hadi Jumanne ijayo yaani tarehe tatu Novemba ambapo aghalabu ya vikao hivyo vinafanyika kwa njia ya intaneti ili kuzuia maambukizi ya corona.

Shakhsia 167 wa ulimwengu wa Kiislamu kutoka nchi 47 pamoja na washiriki wengine 120 wa ndani wanatarajiwa kuhutubia katika mkutano huo ambao mara hii nara na kaulimbiu yake ni 'Ushirikiano wa Kiislamu Wakati wa Maafa na Majanga'.

Miongoni mwa ajenda kuu zinazotarajiwa kujadiliwa katika mkutano wa mara hii ni ushirikiano wa Kiislamu katika kukabiliana na majanga na masaibu, usaliti wa Wamagharibi kwa matukufu ya Palestina, nafasi ya mhimili wa muqawama katika kusambaratisha taathira za kuanzisha baadhi ya mataifa ya Kiarabu uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel na kadhalika mchango wa kamanda mkubwa wa Uislamu Luteni Jenerali Qassim Suleimani katika kuleta umoja na usalama wa ulimwengu wa Kiislamu.

 

Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu hufanyika kila mwaka kwa mnasaba wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Wiki ya Umoja wa Kiislamu ni kipindi cha kati ya tarehe 12 na 17 za Mfunguo Sita Rabiu Awwal kipindi ambacho kinasadifiana na kuadhimisha Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Bwana Mtume SAW.

Tags

Maoni