Oct 31, 2020 10:37 UTC
  • Iran yatoa mkono wa pole kwa serikali na wananchi wa Uturuki kwa maafa ya zilzala ya Izmir

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mkono wa pole kwa serikali na wananhi wa Uturuki kufuatia tetemeko la ardhi lililotokea jana Ijumaa katika eneo la Izmir na kutangaza kuwa Iran iko tayari kwa ajili ya misaada ya aina zote kwa waathiriwa wa janga hilo.

Rais Hassan Rouhani amesema katika ujumbe aliomtumia mwenzake wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan hii leo Jumamosi kwamba amesikitishwa sana na tetemeko la ardhi lililosababisha maafa katika eneo la Izmir na vifo vya watu vilivyosababishwa na janga hilo na amemuomba Mwenyezi Mungu kuzipa subira familia za wahanga wa janga hilo na shifaa kwa majeruhi wa tetemeko hilo.

Rais Rouhani pia amesema kuwa Iran iko tayari kutuma misaada ya aina mbalimbali ikiwemo ya matibabu katika maeneo yaliyoathiriwa na tetemeko hilo na kuongeza kuwa, ana matumaini hali ya amani na utulivu itarejeshwa haraka katika maeneo hayo. 

Rais Hassan Rouhani

Awali Waziri wa Mashauri ya Kigeni, Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Afya, Saeed Namaki na Spika wa Bunge la Iran Muhammad Qalibaf walikuwa tayari wametuma salamu za mkono wa pole kwa wenzao wa Uturuki kutokana na maafa ya tetemeko la ardhi la Izmir.

Eneo hilo lililoko magharbi mwa Uturuki jana Ijumaa lilikumbwa na mitetemeko kadhaa ya ardhi iliyofikia ukubwa wa 6.6 kwa kipimo cha Rishta. Watu wasiopungua 24 wameripotiwa kuaga dunia hadi sasa na wengine zaidi ya 804 wamjeruhiwa. Timu za uokoaji zinaendelea kutafuta manusura chini ya vifusi vya nyumba na majengo yaliyobolewa na mtetemeko huo wa ardhi. 

Tags

Maoni