Nov 14, 2020 08:18 UTC
  • Iran yapuuzilia mbali madai ya kuuawa kinara wa al-Qaeda hapa nchini

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu Iran amekanusha vikali habari za kipropaganda zinazodai kuwa kiongozi wa ngazi za juu wa mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda ameuawa hapa nchini.

Saeed Khatibzadeh amepuuzilia mbali madai hayo yasiyo na msingi na kusisitiza kuwa, nchi hii si mwenyeji wa wanachama wowote wa kundi la wapiganaji wa al-Qaeda.

Khatibazadeh amevionya vyombo vya habari vya Marekani, dhidi ya kutumbukia katika senario za filamu za Hollywood zinazotayarishwa na kusambazwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza bayana kuwa, vyombo vya habari havipaswa kuwa kipaza sauti cha White House cha kueneza habari za urongo na zisizo na msingi wowote.

Ameongeza kuwa, madai ya namna hiyo bila shaka yanaenda sambamba na vita vya kisaikolojia, kihabari na kiuchumi dhidi ya wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu.

Gazeti la Marekani la New York Times huku likinukuu maafisa wasiojulikana wa Marekani, limedai kuwa maajenti wa utawala wa Kizayuni wa Israel hapa nchini walimuua kwa kumpiga risasi kamanda nambari mbili wa kundi la al-Qaeda na mjane wa mtoto wa kiume wa Osama Bin Laden, miezi mitatu iliyopita hapa jijini Tehran.

Ayman al-Zawahri, kinara wa al Qaeda

Gazeti hilo limemtaja kamanda huyo wa al-Qaeda kama Abdullah Ahmed Abdullah, almaarufu kama Abu Muhammad al-Masri, anayedaiwa kuwa alipaswa kurithi mikoba ya kinara wa sasa wa genge hilo, Ayman al-Zawahri.

Hata hivyo Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu Iran anasisitiza kuwa, al-Qaeda ni matunda ya sera ghalati za Marekani na Israel katika eneo la Asia Magharibi, na kwamba Washington na Tel Aviv kwa mara nyingine tena zinatumia habari za upotoshaji ili kuficha mapungufu yao na kueneza chuki dhidi ya Iran.

 

 

Tags