Nov 21, 2020 10:36 UTC
  • Kuongezeka nguvu ya kiulinzi ya Iran katika kivuli cha mashinikizo ya juu kabisa ya Marekani

Siasa imara na za busara za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mkabala na Marekani zimepelekea siasa laini na ngumu za Washington kukabiliwa na changamoto kubwa.

Wakati alipoingia madarakani huko White House mwaka 2016, Rais Donald Trump alianzisha siasa za mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siasa ambazo zilienda sambamba na vitisho vya kijeshi, lakini baada ya kupita miaka minne ya utawala wake mbinu hiyo haijafanikiwa kufikia malengo aliyoyakusudia dhidi ya Iran. Mashinikizo ya juu kabisa, vikwazo juu ya vikwazo na vitisho vya kijeshi ni sera kuu ambayo imekuwa ukifuatwa na serikali ya Trump dhidi ya Iran katika miaka hii miine yya utawala wake. Pamoja na hayo mbinu hiyo haijailazimisha Iran kuketi kwenye meza ya mazungumzo na Marekani wala kuifanya nchi hiyo ichukue hatua yoyote ya kipumbavu kijeshi dhidi ya Iran.

Kwa kutekeleza mashinikizo ya juu zaidi na vikwazo eti vya kulemaza dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, Marekani ilikusudia kuilazimisha Iran iketi kwenye meza ya mazungumzo na kukubali yafanyike mazungumzo mapya ya nyuklia lakini ukakamavu wa kiwango cha juu kabisa na diplomasia imara na ya busara ya Tehran katika uwanja huo imempelekea Trump aendelee kubakia kwenye ndoto yake ya eti kuilazimisha Iran isalimu amri mbele yake.

Katika uwanja huo, jarida la Marekani la National Interest liliandika Alkhamisi kwamba siasa za Marekani za mashinikizo ya juu kabisa zimefanikiwa kwa kiwango cha chini kabisa na hivyo Marekani inapasa kubadilisha siasa zake hizo mkabala na Iran.

Jarida la National Interest

Serikali ya Trump ilikuwa imekusudia kuilazimisha Iran iketi kwenye meza ya mazungumzo kwa ajili ya kujadiliana nayo kuhusu mipango yake ya makombora, ulinzi na siasa zake za eneo, jambo ambalo ni mstari mwekundu kwa Tehran. Ni wazi kuwa hakuna nchi yoyote duniani inayoanika siri zake za ulinzi mbele ya nchi nyingine na kwa kawaida mataifa hupanga mipango yao ya ulinzi kwa kuzingatia hali ya maeneo yao.

Kuhusu suala hilo, Brigedia Jenerali Hussein Dehqani, mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya ulinzi alisema Alkhamisi kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitafanya mazungumzo na yeyote na kwa masharti yoyote yale kuhusu nguvu zake za kijeshi.

Mbali na hayo, hatua madhubuti na imara za Iran zimeipelekea Marekani ikwame katika kuiandama Tehran katika ngazi za kimataifa na hivyo kuifanya nchi hiyo itengwe na jamii ya kimataifa katika uwanja huo. Marekani kushindwa kuungwa mkono na wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika juhudi zake za kurefusha vikwazo vya silaha dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mfano wa wazi kabisa katika uwanja huo.

Kushindwa huko kwa utawala wa Trump mkabala na Iran bila shaka kunatokana na siasa za kujitegemea na kujitawala Iran pamoja na nguvu zake za kijeshi. Hata kama mashinikizo ya kiuchumi ya Marekani yamewaathiri wananchi wa Iran lakini ni wazi kuwa kutegemea uwezo wa ndani kumeifanikisha kupita salama na kuweka nyuma kipindi hicho kigumu.

Brigedia Jenerali Hussein Dehqani

Uwezo mkubwa wa kiulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni dalili ya nguvu ya kijeshi iliyonayo Iran katika kuzuia mashambulizi ya adui, uwezo ambao unatokana moja kwa moja na vipawa vya ndani ya nchi. Makombora mengi na tofauti iliyonayo Iran ni jambo linalofanya hujuma yoyote ya adui kuwa ngumu.

Sisitizo la Marekani la kuondelea kutoa mashinikizo ya juu kabisa na kuogopa kutekeleza mashambulio ya kijeshi dhidi ya Iran bila shaka ni suala linalotokana na kutotabirika vyema matokeo ya hatua kama hiyo. Katika uwanja huo, Brigedia Jenerali Hussein Dehqani, mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya ulinzi amesema: Mapigano madogo tu na ya kitaktiki yanaweza kuibua vita vikubwa na vya pande zote na bila shaka Marekani haina uwezo wa kusimama mbele ya mgogoro kama huo.

Tags