Nov 22, 2020 04:13 UTC
  • Iran: Shambulio la kigaidi la Kabul ni mfano wa vita vya niaba vya Marekani nchini Afghanistan

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, shambulio la kigaidi la Kabul ni mfano mmojawapo wa vita vya niaba na hatua zinazochukuliwa na waitifaki wa utawala wa kigaidi wa Marekani nchini Afghanistan.

Saeed Khatibzadeh amelaani shambulio la kigaidi la mjini Kabul sambamba na kulengwa kwa maroketi kadhaa majengo ya kidiplomasia yaliyoko katika mji mkuu huo wa Afghanistan, ikiwemo sehemu ya ua wa ubalozi wa Iran na akasisitiza kwamba: Utawala wa Marekani ndio unaobeba dhima ya moja kwa moja ya shambulio hilo.

Khatibzadeh ametuma salamu za rambirambi za kuwafariji wananchi na serikali ya Afghanistan hasa familia za waathirika wa shambulio hilo la kigaidi na akaeleza kwamba, katika shambulio la makombora lililolenga maeneo kadhaa ya mji wa Kabul likiwemo eneo la majengo ya kidiplomasia la mji huo, uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa kwa uchache roketi moja limelenga ua wa ndani ya jengo la ubalozi wa Iran.

Hali ya hamkani baada ya shambulio la maroketi mjini Kabul, Afghanistan

Kwa mujibu wa taarifa ya ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Afghanistan, bahati nzuri roketi hilo lililoangukia ndani ya ua wa jengo la ubalozi halikusababisha maafa ya roho za watu, lakini vipande kadhaa vya roketi vimelenga jengo kuu la ubalozi huo na kuharibu vioo na vifaa mbalimbali vya ubalozi.

Maeneo kadhaa ya mji mkuu wa Afghanistan, Kabul jana Jumamosi yalishambuliwa kwa maroketi yapatayo 23, ambapo kwa mujibu ripoti za awali raia wasiopungua saba wameuawa na makumi ya wengine wamejeruhiwa.

Kundi la Taliban limekanusha kuhusika na shambulio hilo.../

Tags