Nov 22, 2020 09:39 UTC
  • Majibu ya Iran kwa upayukaji na tuhuma za nchi za Ulaya zilizomo kwenye JCPOA

Baada ya Marekani kujitoa katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA hapo tarehe 8 Mei 2018 na kuirejeshea Iran vikwazo vyote vilivyoondolewa baada ya mapatano hayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilisubiri mwaka mzima kuona wanachama waliobakia ndani ya JCPOA hasa nchi tatu za Ulaya, watachukua hatua gani za kukabiliana na ubeberu huo wa Marekani, lakini hakuna walichofanya.

Nchi hizo tatu za Ulaya zilizobakia ndani ya JCPOA ambazo ni Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, si tu zimeshindwa kutimiza ahadi zao ndani ya mapatano hayo ya kimataifa, lakini pia zimekataa kukabiliana na ubeberu wa Marekani wa kujitoa katika makubaliano hayo na kuirejeshea Iran vikwazo, kinyume kabisa na vinavyosema vipengee vya JCPOA. Baada ya kusubiri kiasi chote hicho, Tehran nayo iliamua kuchukua hatua za awamu tano za kupunguza ahadi zake ndani ya JCPOA kama majibu yake kwa vitendo vya kiuadui vya Marekani na vya nchi za Ulaya vya kushindwa kutimiza ahadi zao ndani ya mapatano hayo kwa madai ya eti ya kujiepusha na vikwazo vya Marekani. Kichekesho kikubwa ni kuona kuwa nchi hizo tatu za Ulaya za Uingereza, Ujerumani na Ufaransa, badala ya kuilaumu Marekani na pia kubeba zenyewe lawama za kutotekeleza ahadi zao, ndio kwanza zinailaumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa hatua zake za kupunguza ahadi zake ndani ya JCPOA wakati hayo ni majibu ya kawaida kabisa kwa siasa za Marekani na nchi hizo za Ulaya tena baada ya Tehran kuvumilia mwaka mzima.

Katika tamko lao kwa Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, nchi hizo tatu za Ulaya zimeitaka Iran irejee haraka katika hali iliyokuwa nayo kabla ya awamu tano za kupunguza ahadi zake ndani ya JCPOA. 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Saeed Khatibzadeh

 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Saeed Khatibzadeh alisema siku ya Ijumaa kwamba Tehran inalaani tamko hilo la nchi tatu za Ulaya na inasisitiza kwamba shughuli za nyuklia za Iran ni za amani kikamilifu na zinafanyika kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Dk Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alipohojiwa hivi karibuni na gazeti liitwalo "Iran" la hapa nchini Iran amesema: "Sababu zilizoifanya Jamhuri ya Kiislamu ifikie uamuzi wa kupunguza ahadi zake ndani ya JCPOA ni kwamba Marekani imevunja mapatano hayo, na nchi za Ulaya nazo zimekataa kutekeleza ahadi zao 11 zilizotolewa na nchi hizo baada ya Marekani kujitoa katika makubaliano hayo. Kifungu cha 36 cha mapatano hayo kinairuhusu Iran kupunguza ahadi zake, hivyo hatua hizo za Iran zimechukuliwa kwa mujibu wa sheria na vipengee vya JCPOA lakini bado Tehran ni mwanachama wa makubaliano hayo.

Ni jambo lililo wazi kwamba kama litazuka swali kuhusu nani aliviacha vipengee vya mapatano ya JCPOA na kujisalimisha mbele ya mashinikizo ya Marekani, basi upande huo ni wa nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ujerumani na Ufaransa; na kama vipengee vya JCPOA vitadharauliwa mbele ya ubeberu wa Marekani, basi fursa ya kuyalinda makubaliano hayo muhimu ya kimataifa, zitapotea.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Dk Mohamed Javad Zarif

 

Gergio Kafiro, mkurugenzi mtendaji wa chuo cha "Taasisi ya Mashariki ya Kati" cha mjini Washington Marekani anasema: Hatua zilizochukuliwa na Iran zimelenga kutoa ujumbe kwa nchi za Ulaya kwamba kushindwa nchi hizo kukabiliana na vikwazo vilivyorejeshwa na Marekani kuna madhara yake na kwamba nchi za Ulaya zinapaswa kuwa huru katika maamuzi yao na ziache kuitegemea Marekani.

Cha kuchekesha zaidi ni kwamba, nchi tatu za Ulaya zilizomo kwenye mapatano ya JCPOA zinajifanya kama vile zimetekeleza kikamilifu, tena kila kipengee cha mapatano hayo na ndio maana zinajipa haki ya kuilaumu Iran wakati ambapo ni Iran ndiyo iliyotekeleza kikamilifu mapatano ya JCPOA kwa ushahidi  wa ripoti chungu nzima za Wakala wa Kimataifa wa Nishati wa Atomiki, wakati nchi za Ulaya hazijatekeleza hata ahadi yao moja. Ni wazi kuwa, msimamo wa hivi sasa wa nchi hizo za Ulaya kuhusu JCPOA hautokuwa na matunda mengine zaidi ya kupoteza imani na kuharibu anga ya mazungumzo na ushirikiano iliyojitokeza baada ya kufikiwa makubaliano ya JCPOA.