Nov 22, 2020 12:35 UTC
  • Khatibzadeh: Yeyote atakayekuweko White House hatakuwa na chaguo isipokuwa kuheshimu haki za taifa la Iran

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, yeyote atakyekuweko Ikulu ya White House hatakuwa na chaguo jengine isipokuwa kuheshimu haki za taifa la Iran.

Saeed Khatibzadeh ameyasema hayo leo katika mkutano na waandishi wa habari alipojibu suali kuhusu kurudi tena Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA baada ya Joe Biden kuingia madarakani na masharti ya Iran juu ya suala hilo. Khatibzadeh amesisitiza kuwa: yeyote atakayekuweko Ikulu ya White House hatakuwa na chaguo jengine isipokuwa kuheshimu haki za taifa la Iran.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza pia kwamba, Tehran haina mzaha na mtu yeyote kuhusu usalama wake wa taifa na akasisitiza kuwa, maslahi ya taifa na usalama wa taifa ni suala muhimu kwa Iran, kwa hiyo popote pale vitakapohatarishwa Tehran itatoa jibu kali wakati wowote na mahali popote pale.

Saeed Khatibzadeh amebainisha pia kuwa, sera za mashinikizo ya juu ya kabisa zimepelekea kushindwa kwa kiwango cha juu kabisa Marekani na akasisitiza kwamba, utawala wa sasa wa Marekani hauwezi kuendeleza sera zake zilizoshindwa na kugonga mwamba.

Amesisitizia pia kuendelezwa muqawama kwa asilimia mia moja katika medani zote dhidi ya Israel na akakumbusha kuwa Iran iko nchini Syria kwa ajili kutoa ushauri wa kijeshi, kwa hivyo yeyote atakayefanya chokochoko dhidi ya uwepo huo atakabiliwa na jibu kali.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani pia safari ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu zilizopewa jina la Israel, ambapo mbali na kusisitizia msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu wa kuendelea kuunga mkono malengo matukufu ya Palestina amesema, usaliti uliofanywa na baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu na hatua zinazochukuliwa bila aibu na utawala ulioko sasa katika Ikulu ya White House ni pande mbili za sarafu moja.../

Tags