Nov 25, 2020 03:17 UTC
  • Chanjo za corona za Iran zasajiliwa katika Shirika la Afya Duniani

Katibu wa kamati ya sayansi ya tume ya taifa ya kukabiliana na corona nchini Iran amesema, chanjo za ugonjwa wa Covid-19 zilizotengenezwa hapa nchini zimesajiliwa katika Shirika la Afya Duniani (WHO).

Mostafa Qanei ameliambia shirika la habari la IRNA kwamba, kuna aina kadhaa za chanjo za corona ambazo zinaendelea kutengenzwa hapa nchini ambazo baadhi yao zimefanyiwa majaribio kwa mafanikio kwa wanyama na baadhi yao zinakaribia kukamilisha awamu hiyo.

Qanei amebainisha kuwa, watafiti wa Kiirani wamefanikiwa kuufikia utalaamu wa utengenezaji wa chanjo ya corona unaotumika duniani kwa kutumia njia tofauti na hivi sasa wanafanya jitihada kadiri ya uwezo wao kuhakikisha wanafikia lengo la uzalishaji wa chanjo hiyo.

Katibu wa kamati ya sayansi ya tume ya taifa ya kukabiliana corona ameongeza kuwa, kuna uwezekano mkubwa chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 iliyotengenezwa hapa nchini itakuwa tayari kwa matumizi ufikapo msimu wa joto wa mwaka ujao utakaoanza mwezi Juni na wananchi wataweza kuipata kwa ajili ya kinga ya ugonjwa huo.

Waziri wa Afya wa Iran Saeed Namaki

Waziri wa Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu wa Iran Saeed Namaki alitangaza siku ya Jumatatu kuwa, mashirika manne ya Iran yanashughulika na kazi ya utengenezaji chanjo ya corona na kuna matumaini kibali cha kuifanyia majaribio chanjo hiyo kwa binadamu kikatolewa leo Jumatano.

Idadi ya watu waliopatwa na virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19 duniani kote hadi sasa imefikia watu wapatao milioni 60, ambapo watu wasiopungua 1,403,000 miongoni mwao wamefariki dunia kwa ugonjwa huo.../