Nov 25, 2020 07:41 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Basij ni utajiri mkubwa na hazina liliyotunukiwa na Mungu taifa la Iran

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, jeshi la kujitolea la Basij ni utajiri mkubwa na hazina liliyotunukiwa na Mwenyezi Mungu taifa la Iran.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo kwa mnasaba wa maadhimisho ya kuasisiwa jeshi la kujitolea la wananchi la Basij.

Katika ujumbe na salamu maalumu alizotoa kwa mnasaba huo, Ayatullah Khamenei amesema, Basij ni kumbukumbu adhimu na ing'arayo iliyoachwa na Imam Khomeini (MA), dhihirisho la nguvu na uwezo wa kitaifa na onyesho la upendo, ikhlasi, basira na juhudi kubwa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha kuwa, katika kuilinda nchi, kujitawala kwake na uthabiti wake, katika utoaji huduma zenye umuhimu mkubwa na kwa wigo mpana nchini, katika harakati za maendeleo ya sayansi na teknolojia mpya, katika masuala ya thamani za kiakhlaqi na kujenga mazingira ya kimaanawi, kote huko jina la Basij linatumika na ushiriki wa Basij unashuhudiwa.

Askari wa jeshi la kujitolea la wananchi la Basij

Katika sehemu nyingine ya ujumbe wake huo, Ayatullah Khamenei amesema, azma na imani, kuhisi kuwa na masuulia na kujiamini ni misingi mikuu ya kujengea uwezo na kutatua matatizo; na akaongezea kwa kusema: Yote haya ni neema na atiya za Mwenyezi Mungu ambazo inapasa zihifadhiwe na kudumishwa kwa kumshukuru Mola na kuendelea kuzitunza daima.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, Basij ni utajiri mkubwa na hazina liliyotunukiwa na Mwenyezi Mungu taifa la Iran na akabainisha kwamba, maadui wa taifa hili hivi sasa na daima wamekuwa na wataendelea kufikiria jinsi ya kuufuta utajiri na hazina hiyo au kuzifanya zisiwe na taathira.

Ayatullah Khamenei amesisitiza pia kwamba, viongozi wa jeshi lenyewe na mabasij wote azizi, kila mmoja ajihisi ana jukumu la kuvunja hila na vitimbi vya adui na kuweza kupiga hatua mbele kwa mipango maalumu na kwa ikhlasi na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu.../

Tags