Nov 25, 2020 12:19 UTC
  • Rais Rouhani: Serikali ijayo ya Marekani ifidie makosa yaliyotangulia

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria ushindi wa wananchi wa Iran na kushindwa adui katika vita vyake vya kiuchumi dhidi ya taifa hili na kueleza kwamba, serikali ijayo ya Marekani inapaswa kulaani waziwazi sera na hatua zisizo za kibinadamu na kigaidi za Donald Trump na ifidie siasa hizo zisizo sahihi.

Rais Rouhani amesema hayo leo katika kikao na baraza lake la mawaziri ambapo sambamba na kusifu muqawama na kusimama kidete wananchi wa Iran katika vita vya kiuchumi amesema bayana kwamba, moja ya madhihirisho makubwa ya ushindi wa taifa la Iran na kushindwa adui kusiko na shaka katika vita vya kiuchumi ni kumalizika kipindi cha 'u-trump' (Trumpism).

Dakta Hassan Rouhani ameashiria kumalizika kipindi cha utawala wa Rais Donald Trump na jinai zake alizofanya dhidi ya taifa la Iran na kukumbusha kwamba, Trump amefanya jinai mbaya kabisa katika historia dhidi ya serikali na mataifa huru kama Iran na Palestina.

Joe Biden, Rais mteule wa Marekani

 

Rais wa Iran amesema kuwa, kupata pigo Trump katika majukwaa ya kimataifa, asasi za kisheria, kufeli kwake katika vigezo vya kimaadili, kutokubaliwa na fikra za waliowengi ulimwenguni na fikra za waliowengi ndani ya Marekani kwenyewe ndio sababu zilizomfanya ashindwe katika uchaguzi wa Rais na kuongeza kuwa, serikali ijayo ya Marekani inapaswa kufanya mambo makubwa ili ifidie makosa ya huko nyuma na kurekebisha sura na haiba ya nchi hiyo iliyoharibiwa katika kipindi cha utawala wa Trump.  

Rais Rouhani amezungumzia janga la Corona na kusema kuwa, kwa sasa hakuna njia nyingine yoyote ile ya kukabiliana na virusi hivi isipokuwa kufuata maagizo ya kitiba kama kuosha mikono, kuvaa barakoa, kuchunga utengano wa kijamii sambamba na kutii kanuni zilizowekwa na serikali za kukabiliana na virusi hivi angamizi.

Tags