Nov 27, 2020 12:32 UTC
  • Iran yafafanua mchakato wa kuachiwa huru raia wake 3 kwa kubadilishana na jasusi wa Israel

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa ametoa ufafanuzi kuhusu namna raia watatu wa Iran walivyoachiwa huru mkabala na Jamhuri ya Kiislamu kumwachia jasusi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kylie Moore-Gilbert, mwenye uraia pacha wa Australia na Uingereza, aliyekuwa ameingia Iran kwa lengo la kufanya usausi na kukusanya taarifa nyeti kwa kutumia kichaka cha shughuli za utafiti na uhakiki kuhusu Uislamu, alikamatwa hapa nchini na vikosi vya intelijensia tarehe 21 Septemba 2018.

Baada ya jasusi huyo kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na mahakama alihukumiwa kifungo cha miaka 10 jela kwa kupatikana na hatia ya kufanya vitendo vya kuhatarisha usalama wa taifa kupitia ushirikiano wa kiintelijensia aliokuwa nao na utawala wa Kizayuni; na baada ya kutumikia miaka miwili ya kifungo chake, hatimaye Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu umechukua uamuzi wa kumwachia kwa kubadilishana na raia watatu wa Iran ambao ni wanaharakati wa shughuli za kiuchumi waliokuwa wamekamatwa kwa kisingizio cha ukwepaji vikwazo.

Sayyid Abbas Araqchi

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa, ambaye alishiriki katika shughuli ya kubadilishana raia watatu wa Iran na Muaustralia huyo mwenye uraia pacha wa nchi hiyo na Uingereza iliyofanyika nchini Thailand akisema: Siku ya Jumatano, na kufuatia kazi kubwa ya kidiplomasia iliyofanywa katika kuamiliana na nchi mbili za Thailand na Australia na ambayo ilichukua zaidi ya mwaka mmoja, Wairani watatu waliokuwa wamefungwa jela nchini Thailand waliachiwa huru mkabala na Muaustralia aliyekuwa akitumikia kifungo mjini Tehran.

Araqchi ameongeza kuwa: Mabadilishano hayo yalikuwa ni ya aina ya pekee kwa sababu nchi tatu zilihusika katika mchakato wa muamala wa pande tatu ambapo raia watatu wa Iran waliachiwa huru mkabala wa raia mmoja tu wa kigeni.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amesema, mabadilishano hayo yalifanyika uwanja wa ndege wa Tehran ambapo kwanza raia watatu wa Iran walioachiwa huru kutoka Thailand wakisafiri kwa ndege maalum ya Australia waliwasili na kupokewa mjini Tehran, kisha ndipo mfungwa huyo Muaustralia alipoachiwa na kuondolewa nchini.../

 

Tags