Nov 28, 2020 08:07 UTC
  • Rais Rouhani: Mauaji ya wanasayansi wa nyuklia yanatokana na maadui kushindwa mtawalia

Rais Hassan Rouhani amesema, hapana shaka tukio la kigaidi na la kutapatapa la mauaji ya wanasayansi wa nyuklia linatokana na kushindwa na kuemewa maadui waliolikamia taifa la Iran.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo katika ujumbe aliotuma wa salamu za rambirambi na mkono wa pole kufuatia kuuawa shahidi mwanasayansi wa nyuklia wa Iran Mohsen Fakhrizadeh na akaongeza kuwa, kwa mara nyingine, mikono michafu ya uistikbari wa dunia ikiwatumia vibaraka wa utawala ghasibu wa Kizayuni imetapakaa damu ya mmoja wa wana mashujaa na wakomavu wa ardhi hii na hivyo kuliingiza taifa la Iran kwenye huzuni na majonzi ya kuondokewa na mwanasayansi mwenye idili kubwa.

Rais Rouhani amesisitiza kuwa, hapana shaka tukio la kigaidi na la kutapatapa la mauaji ya wanasayansi wa nyuklia linatokana na kushindwa na kuemewa maadui waliolikamia taifa la Iran, katika kukabiliana na harakati ya kielimu, mafanikio ya kujivunia na uwezo wa taifa adhimu la Iran; pamoja na kushindwa kwao mtawalia katika eneo na katika nyuga zingine za kisiasa duniani. Ameongeza kuwa mauaji hayo yamedhihirisha tena upeo wa uovu na uadui wao mbele ya macho wa walimwengu kama zilivyo hatua zao zingine za kinyama.

Shahidi Mohsen Fakhrizadeh

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, maadui woga wa taifa wa Iran wajue kwamba kumuua shahidi Mohsen Fakhrizadeh hakutateteresha hata kidogo irada ya vijana na wanasayansi wa Iran ya Kiislamu ya kushikamana na njia ya ustawi wa kasi wa kielimu na kufikia kwenye vilele vya mafanikio ya kujivunia; lakini badala yake yatawafanya wawe na azma thabiti zaidi ya kuendeleza njia ya shahidi huyo mwenye hadhi kubwa; na damu za mashahidi wa Iran zitaendelea kubakia zikichemka na kutiririka.

Mohsen Fakhrizadeh, Mkuu wa Shirika la Utafiti na Ubunifu la Wizara ya Ulinzi ya Iran aliuawa shahidi jana jioni katika shambulio li kigaidi lililofanywa kandokando ya mji wa Tehran.../

 

Tags