Nov 28, 2020 09:42 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Watieni adabu waliofanya na kuamrisha jinai ya kuuliwa kigaidi shahid Fakhrizadeh

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo wajibu wa kutiwa adabu na kupewa adhabu isiyoepukika wote waliofanya na kuamrisha mauaji ya kigaidi ya mwanasayansi wa Kiirani, Dk. Mohsen Fakhrizadeh.

Mapema leo asubuhi, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametuma ujumbe wa pongezi na tanzia kufuatia kuuawa shahidi na kumpoteza mwanasayansi bingwa aliyebobea katika masuala ya nyuklia na ulinzi wa Iran, Dk Mohsen Fakhrizadeh na amesisitiza kutolewa adhabu isiyoepukika kwa waliofanya na walioamrisha jinai hiyo na wajibu wa kuendelezwa jitihada za kielimu na kiufundi za shahid Fakhrizadeh.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika ujumbe wake huo kwamba: Mwanasayansi huyu bingwa wa nyuklia na masuala ya ulinzi ambaye ameuliwa shahidi na mamluki watenda jinai na wenye nyoyo ngumu, ametoa roho yake azizi na yenye thamani kubwa katika njia ya Allah kupitia jitihada zake kubwa za kielimu na za kubakia milele na hivyo amefanikiwa kupata daraja ya juu ya kuuawa shahidi ikiwa ni zawadi kutoka kwa Mola wake.

Mohsen Fakhrizadeh, Mkuu wa Shirika la Utafiti na Ubunifu la Wizara ya Ulinzi ya Iran aliuawa shahidi jana jioni katika shambulio la kigaidi lililofanywa katika viunga vya jiji la Tehran.

Tags