Nov 28, 2020 11:04 UTC
  • Mauaji ya kigaidi ya Mohsen Fakhrizadeh; kukaririwa senario iliyofeli ya kuzuia ustawi wa kielimu nchini Iran

Mohsen Fakhrizadeh ambaye alikuwa Mkuu wa Shirika la Utafiti na Ubunifu la Wizara ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliuawa Ijumaa alasiri katika moja ya viunga vya mji mkuu, Tehran.

Hii si mara ya kwanza kwa msomi wa Kiirani kuuliwa na magaidi. Kulengwa kigaidi wasomi wa Kiirani katika kipindi cha miaka michahe iliyopita, kunatufanya tujiulize maswali mawili muhimu nayo ni kwamba je, ni nini hasa malengo ya magaidi kuwalenga wasomi hao na hasa wale wanaojishughulisha na masuala ya nyuklia? Swali la pili ni kuwa je, ni serikali au taasisi zipi zinazopanga njama za kuwaua kigaidi wasomi wa Iran na ni nani wanashirikiana nao katika kutekeleza njama hizo?

Bila shaka moja ya malengo hayo ni kusimamishwa mwenendo wa ustawi wa kieleimu wa Iran na hasa katika sekta ya ulinzi na teknolojia ya nyuklia. Wairani waliouawa ni wasomi ambao hawakuwa tishio kwa nchi nyingine. Sababu pekee ya kuuawa kwao ni maadui kuogopa vipawa vyao vya kielimu na maendeleo ya taifa la Iran. Shahidi Mohsen Fakhrizadeh amekuwa mmoja wa wasomi na wanasayansi mashuhuri wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye alikuwa ameorodheshwa kwenye orodha ya watu 500 bora  na wenye nguvu duniani kwa mujibu wa jarida la Marekani la Foreign Policy.

Gari alimokuwa ndani yake Mohsen Fakhrizadeh wakati aliposhambuliwa na magaidi

Ama katika kujibu swali la pili ni lazima tuseme kuwa utawala haramu wa Israel kabla ya mauaji haya ya kigaidi tayari ulikuwa imetekeleza mauaji mengine ya kigaidi dhidi ya wanasayansi wa Iran wanaojishughulisha na masuala ya nyuklia, wakiwemo Manuchehr Shahriyari na Masoud Ali Muahammadi. Mauaji ya kigaidi ya Mohsen Fakhrizadeh pia yanachambuliwa na vyombo vya habari vya kimataifa kwa mtazamo huo huo. Kanali ya televisheni ya al-Mayadeen mara tu baada ya kuuliwa kigaidi Mohsen Fakhrizadeh, ilinukuu vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vikisema kuwa watawala wa Tel Aviv wamehusika katika mauaji hayo hasa kutokana na matamshi ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala huo aliyesema kwamba wiki hii alikuwa amefanya kazi nyingi ambazo hangeweza kuzitaja zote.

Ronn Bergman mwandishi na mchambuzi wa masuala ya usalama wa Israel Machi 2019 alifichua kwamba shirika la ujasusi la utawala haramu wa Israel Mosad, lilikuwa limeainisha wasomi 15 wa Iran ambapo 6 kati yao walilengwa na kuuawa kwa mabomu yaliyotegwa kwenye magari yao asubuhi walipokuwa njiani kwenda kazini.

Nalo jarida la kila wiki  la Spiegel la Ujerumani liliandika baada ya kuuawa shahidi Daryoush Ridhaiyan kwamba mauaji ya kigaidi ya wasomi wa Iran yanatekelezwa na shirika la Mosad.

Kuwekwa majina ya wanasayansi wa Iran waliouawa kigaidi, katika ripoti za siri za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA na kisha mashirika ya ujasusi ya Israel kupewa ripoti hizo, ni suala jingine muhimu ambalo lilipelekea mashirika hayo kuwaua kigaidi wasomi hao wa Iran katika kipindi hicho.

Seymour Hersh mwandishi habari na mchambuzi wa Marekani huku akisema kuwa kuua wasomi wa Iran ni njama ya pamoja inayotekelezwa na Israel pamoja na Marekani ameandika kwamba kwa muda mrefu Marekani imekuwa ikiwapa wanachama wa kundi la Munafiqeen la Iran katika jangwa la Nevada, mafunzo ya jinsi ya kutekeleza operesheni za kigaidi na uharibifu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika hali ambayo nchi zinazodai kupambana na ugaidi kila zinapopata fursa, huwa hazisiti hata sekunde moja kuituhumu Iran kuwa inahusika na ugaidi na kuvuruga usalama katika eneo, mara hii tunapasa kusubiri kuona iwapo jamii ya kimataifa itachukua hatua yoyote ya kulaani mauaji haya ya kigaidi dhidi ya msomi wa Iran au la.

Pamoja na ha hayo, lakini wasomi na wanasayansi wa Iran wamethibitisha kivitendo kuwa hawatatishwa na ugaidi na jinai za kikatili zinazotekelezwa na maadui kwa lengo la kuwazuia wafikie malengo yao matukufu, iwe ni mauaji ya kinyama na kigaidi kama yale yaliyotekelezwa dhidi ya Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), aliyekuwa mstari wa mbele katika kupambana na ugaidi unaodhaminiwa kwa hali na mali na Marekani, Israel na Saudi Arabia au yale yaliyotekelezwa dhidi ya wasomi wa Iran katika sekta za teknolojia na ulinzi. Bila shaka jinai hizo zitafuatiliwa kwa karibu na jibu muwafaka kutolewa.

Hata kama kumpoteza msomi na mwanasayansi mashuhuri kama Mohsen Fakhrizadeh ni tukio chungu kwa taifa la Iran, lakini ni wazi kuwa wapangaji wa jinai hiyo ya kigaidi wamefanya kosa kubwa la kimahesabu kwani ustawi wa kielemu na kiteknolojia nchini hapa unatokana na vyanzo vya ndani na bila shaka njia ya mashihidi hao wa elimu itadumishwa kwa azma, moyo thabiti na nguvu kubwa zaidi.