Dec 02, 2020 02:31 UTC

Mjumbe wa kamati ya uongozi ya Bunge la Iran amesema idadi kubwa ya wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA waliokuwako hapa nchini walikuwa majasusi na walilipatia Shirika la Ujasusi la Marekani CIA taarifa za wanasayansi wa Iran.

Ahmad Amir Abadi Farahani, mjumbe wa kamati ya uongozi ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu amepuuzilia mbali msimamo uliotangazwa na Mkurugenzi Mkuu wa IAEA kwamba hakuna yeyote atakayenufaika kwa kusimamishwa shughuli za ukaguzi nchini Iran na kueleza kwamba, Iran ilikubali na kujitolea kwa hiari yake kutoa ushirikiano na kutekeleza Protokali ya Ziada ya Mkataba wa Nyuklia, lakini aghalabu ya wakaguzi wa IAEA ni majasusi wa CIA ambao wamekuja Iran chini ya mwavuli wa wakala huo wa atomiki, na baadhi yao wamegunduliwa na kutiwa mbaroni.

Amir Abadi amesisitizia ulazima wa kukomeshwa ujasusi unaofanywa na wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki nchini Iran.

Kikao cha bunge la Iran 

Kufuatia ombi la wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran la kutaka wakaguzi wa IAEA walioko hapa nchini watimuliwe, Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa wakala huo wa kimataifa wa nishati ya atomiki amesema, hakuna mtu yeyote atakayenufaika kwa kupunguzwa, kuwekewa mpaka au kuvurugwa mashirikiano ya IAEA na Iran.

Kwa mujibu wa mpango uliopendekezwa na bunge la Iran wa kuchukua 'hatua ya kistratejia ya kuondoa vikwazo na kulinda maslahi ya taifa la Iran', endapo katika muda wa mwezi mmoja baada ya kupitishwa sheria ya mpango huo nchi wadau wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA hazitatekeleza ahadi na majukumu yao; ikiwa mahusiano ya kibenki hayatorejea katika hali ya kawaida na endapo vizuizi vya usafriishaji na uuzaji mafuta na bidhaa za mafuta za Iran havitaondolewa kikamilifu na fedha zinazotokana na mauzo hayo kurejeshwa kikamilifu na kwa haraka, serikali ya Jamhuri ya Kiislamu itawajibika kusimamisha utekelezaji wa hati ya Protokali ya Ziada.../

Tags