Dec 02, 2020 02:39 UTC
  •  Rouhani atuma ujumbe UN; aitolea wito jamii ya kimataifa kukabiliana na utawala wa Kizayuni

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma ujumbe kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kushikamana na Wananchi wa Palestina na kuitolea mwito jamii ya kimataifa kukabiliana na hatua za utawala wa Kizayuni unaouwa watoto.

Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, sambamba na kuwadia Siku ya Kimataifa ya Kushikamana na Wananchi wa Palestina; jana Jumanne kulifanyika hafla iliyohudhuriwa na wawakilishi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa katika makao makuu ya umoja huo huko New York. 

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana alituma ujumbe kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuashiria namna tarehe 29 Novemba inavyokumbushia kkaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina na utawala wa Kizayuni kwa zaidi ya miongo saba; na kutaabika kila uchao wananchi wa Palestina na kuendelea kudhulumiwa na kushindwa kudhaminiwa haki zao wananchi hao madhulumu wa Palestina na kueleza kuwa: kila siku tunashuhudia kushtadi pakubwa siasa za uvamizi na kibaguzi na jinai zilizoratibiwa za utawala huo ikiwamo kufuatiliwa mpango wa kuyaunganisha maeneo ya Ukingo wa Magharibi na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, kuuliwa shahidi wananchi madhulumu wa Palestina na kuendelea vikwazo dhidi ya haki za binadamu kunakotekelezwa dhidi ya raia wa Ukanda wa Ghaza katika kipindi hiki cha maambukizi ya corona.

Wakazi wa Gaza na mapambano dhidi ya corona 

Amesema raia wa Palestina wanakabiliwa na vizuizi mbalimbali na hivyo    kushindwa kujidhaminia mahitaji ya kitiba na misaada ya kiafya. 

Katika ujumbe wake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Rais Rouhani ameongeza kueleza kuwa: ni dhahir shahir kwamba lengo la kuyahudisha na kuharibu utambulisho wa kihistoria na Kiislamu wa Baitul Muqaddas ni kwa ajili ya kuzikalia ardhi zote za Palestina na kuzuia haki ya kurejea wakimbizi wa Kipalestina katika ardhi zao za mababu. Amesema hatua zote hizo kwa mara nyingine tena zinaweka wazi dhati ya kibaguzi ya utawala huo katika kuzikalia zaidi ardhi za Wapalestina na kupuuza  haki ya wazi na isiyopingika ya raia hao. 

Rais Rouhani ameongeza kuwa: utawala wa Kizayuni kutokana na kuungwa mkono na baadhi ya nchi wanachama wa kudumu ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kila siku unashadidisha jinai na vitendo vyake visivyo vya kibinadamu dhidi ya Wapalestina; na unatekeleza hatua na siasa za uvamizi katika eneo la Mashariki ya Kati khususan kuzivamia nchi za Syria na Lebanon na kuendesha mradi wa siri wa kuunda silaha za maangamizi ya umati na hivyo kuitia hatarini amani na uthabiti wa eneo zima. 

Tags