Dec 02, 2020 09:32 UTC
  • Undumakuwili katika mapambano dhidi ya ugaidi; siasa zitakazopelekea kufeli mapambano hayo

Mapambano dhidi ya ugaidi yanahitajia azma thabiti ya jamii ya kimataifa lakini dalili na mienendo iliyopo inaonyesha wazi kwamba hakuna azma ya aina hiyo kwa sasa katika ngazi za kimataifa.

Je, suala hilo linatokana na nini? Je,taasisi husika katika uwanja huo zimezembea katika utekelezaji wa majukumu yao au ni misimamo ya kundumakuwili ya nchi zinazodai kuongoza mapambano dhidi ya ugaidi ndiyo imepelekea kuongezeka na kuenea ugaidi duniani?

Kazem Gharibabadi, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Taasisi za Kimataifa mjini Vienna Austria Jumanne alimwandikia barua Katibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini humo akilaani vikali kuuliwa kigaidi mwanasayansi wa Iran, Shahidi Mohsen Fakhrizadeh ambaye pia alikuwa Mkuu wa Shirika la Utafiti na Ubunifu la Wizara ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na kulaani vikali siasa za kundumakuwili zinazotekelezwa dhidi ya nchi tofauti duniani. Amesema undumakuwili katika mapambano dhidi ya ugaidi si tu kuwa si jambo zuri bali pia utapelekea kushindwa mapambano ya kimataifa dhidi ya ugaidi.

Kazem Gharibabadi

Sehemu ya barua hiyo imeashiria ugaidi wa utawala haramu wa Israel dhidi ya Iran katika miongo kadhaa iliyopita na pia hatua ya utawala huo ya kuua kigaidi wanasayansi na wasomi katika nchi kadhaa. Barua hiyo inasema: Tunaitaka jamii ya kimataifa kutekeleza wajibu wake katika kulinda sheria za kimataifa za kupambana na ugaidi na wakati huo huo kulaani vikali hatua hizo zisizo za kibinadamu za utawala wa Israel.

Kwa bahati mbaya Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa hazijachukua hatua zozote za maana katika kupambana na ugaidi. Ukweli huo mchungu unaonekana wazi kupitia ukatili na ugaidi unaotekelezwa kila uchao na utawala wa kibaguzi wa Israel dhidi ya Wapalestina, mauaji ya watoto na wanawaek yanayotekelezwa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen na vilevile ugaidi wa pamoja unaotekelezwa na Marekani na Israel katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati). Umoja wa Mataifa umekuwa ukipitisha maazimio ya kulaani kila aina ya ugaidi na kusema kuwa jambo hilo ni jinai isiyokubalika.

Mauaji ya mwanasayansi bora, bingwa na wa kupigiwa mfano wa Iran katika uwanja wa nyuklia na sekta ya ulinzi pia yanapaswa kujumuishwa katika maazimio hayo kwa kulaaniwa vikali mauaji ya kigaidi yaliyotekelzwa dhidi yake na utawala wa Israel. Mohsen Fakhrizadel alikuwa mwanasayansi hodari ambaye kutokana na huduma zake za kielimu na kiutafiti alikuwa na mchango mkubwa katika uwanja wa ulimu na teknoilojia nchini, ukiwemo uzalishaji wa vifaa vya kugundua virusi vya corona pamona ha chanjo ya kukabiliana na maradhi hayo. Ni wazi kuwa kuuawa kwa mwanasayansi huyo kama ulivyo ugaidi mwingine wa kimataifa, ni tishio dhidi ya amani na uslama wa dunia na ni jambo linalokwenda kinyume na misingi ya sheria za kimataifa na hati ya Umoja wa Mataifa.

Shahidi Mohsen Fakhrizadeh, aliyeuawa kigaidi na utawala wa Israel

Ushahidi uliopo unathibitisha wazi kuwa mashirika ya kijasusi ya utawala haramu wa Israel ndiyo yalitekeleza mauaji hayo ya kigaidi kwa ushirikiano na makundi ya kinafiki na kibaraka ya ndani ya nchi. Mwezi Januari mwaka huu Marekani pia ilitekeleza ugaidi wa kimataifa kwa kumuua kikatili Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), nje ya uwanja wa kimataifa wa ndege wa Baghdad Iraq, na ambaye alikuwa amewasili nchini humo kwa mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hiyo. Aliuawa shahidi akiwa na Abu Mahdi al-Muhandis, Naibu Mkuu wa Harakati ya Wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi ya Iraq, pamoja na watu wengine wanane waliokuwa wameandamana nao.

Kuendelea kimya cha jamii ya kimataifa na taasisi husika za kimataifa katika uwanja huo kuna matokeo mawili muhimu: La kwanza ni kukaririwa na kuenea ugaidi duniani na la pili ni taasisi na mashirika ya kimataifa kupoteza heshima na itabari yao.

Ukosoaji uliofanywa na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Taasisi za Kimataifa huko Vienna kuhusu undumakuwili katika mapambano dhidi ya ugaidi unapaswa kutathminiwa katika mtazamo huo.