Dec 03, 2020 08:07 UTC
  • Mauaji ya shahid Fakhrizadeh ni jinai ya wazi ya ugaidi wa kiserikali

Mkuu wa Ofisi ya Uwakilishi ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema mauaji ya mwanasayansi mkubwa wa nyuklia Mohasen Fakhrizadeh ni hatua za kuvunja moyo za kutaka kuhatarisha amani ya kimataifa na ya kikanda na ni jinai ya wazi ya ugaidi wa kiserikali.

Mohammad Reza Sahraei ameyasema hayo katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika kuzungumzia kadhia ya Palestina.

Ameashiria shambulio la kigaidi lililopelekea kuuawa shahidi Mohsen Fakhrizadeh, Mkuu wa Shirika la Utafiti na Ubunifu la Wizara ya Ulinzi ya Iran na kueleza kwamba, mojawapo ya miradi ya karibuni kabisa ya utafiti iliyofanywa na mwanasayansi huyo ni utengenezaji wa kifaa cha mwanzo cha kupimia ugonjwa wa Covid-19 kilichobuniwa nchini Iran.

Sahraei ameashiria pia ushahidi mkubwa uliopo unaothibitisha kuhusika utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika shambulio hilo la kigaidi na akasisitiza ulazima wa jamii ya kimataifa kulaani kitendo hicho.

Katika hotuba yake hiyo, Mkuu wa Ofisi ya Uwakilishi ya Iran katika Umoja wa Mataifa amezungumzia pia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina na kueleza kwamba, kukinzana hatua za utawala ghasibu wa Kizayuni na sheria na taratibu za kimataifa kunakwamisha juhudi za jamii ya kimataifa za kuipatia suluhusho la kiuadilifu na la kudumu kadhia ya Palestina.

Saharei ameongeza kuwa, kuhitimishwa mapigano na machafuko ya zaidi ya miongo saba katika eneo la Asia Magharibi kutawezekana tu kwa kutatuliwa kadhia ya Palestina kwa kukomeshwa ukaliaji wa mabavu wa ardhi hiyo, kurejea wakimbizi Wapalestina katika ardhi yao ya jadi, kuwahakikishia watu wa Palestina haki yao ya wazi kabisa ya kujiamulia mustakabali wao na kuundwa nchi huru ya Palestina, ambayo mji mkuu wake ni Baitul Muqaddas (Jerusalem).../