Dec 03, 2020 11:07 UTC
  • Iran yaishukuru Russia kwa msimamo wake thabiti wa kulaani mauaji ya Fakhrizadeh

Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Russia ameishukuru nchi hiyo kwa msimamo wake imara wa kulaani mauaji ya kigaidi aliyofanyiwa mwanasayansi mkubwa wa nyuklia na masuala ya kiulinzi wa Iran, shahid Mhosen Fakhrizadeh.

Balozi Kazem Jalali amegusia kuanzishwa daftari la kumbukumbu ya shahid Fakhrizadeh huko Moscow, mji mkuu wa Russia na kuongeza kuwa, tukio chungu la kuuliwa kigaidi mwanasayansi huyo wa Iran limeakisiwa sana na vyombo vya habari na wakuu wa kisiasa na kibunge wa Russia pamoja na mabalozi wa nchi za nje walioko nchini humo.

Aidha amesema, ugaidi huo wa kiserikali umelenga kuikwamisha Iran katika maendeleo yake ya kisayansi na kiteknolojia ikiwemo teknolojia ya matumizi ya amani ya nishati yanyuklia na kusisitiza kuwa, ugaidi huo ni uvunjaji wa wazi wa misingi ya kibinadamu na sheria za kimataifa na kwamba ni haki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kulipiza kisasi kiistratijia, jinai na ugaidi huo.

Balozi Kazem Jalali

 

Siku chache zilizopita, Mkuu wa Kamati ya Masuala ya Kigeni ya Bunge la Russia (Duma) alisema kuwa, mauaji aliyofanyiwa mwanasayansi wa nyuklia wa Iran, shahidi Mohsen Fakhrizadeh, ni ya kigaidi yaliyofanywa kwa ajili ya kuichochea Iran ichukue hatua za pupa.

Leonid Slutsky aliandika hayo katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba na kutoa mwito wa kujiepusha na machafuko zaidi katika eneo hili.

Magaidi wenye silaha, siku ya Ijumaa, Novemba 27, 2020 waliishambulia gari la Dk Mohsen Fakhrizadeh, Mkuu wa Taasisi ya Utafiti na Ubunifu katika Wizara ya Ulinzi ya Iran na kumuua shahidi mwanasayansi huyo wa teknolojia ya nyuklia ambaye alikuwa mstari wa mbele pia katika kupambana na ugonjwa wa COVID-19.