Dec 03, 2020 11:08 UTC
  • Rais Rouhani: Wananchi wa Iran wamekabiliana vilivyo na vita vya kiuchumi, kisiasa na kisaikolojia

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amegusia vita vya pande zote vya kiuchumi vilivyoanzishwa na Marekani dhidi ya Tehran na kusema kuwa, wananchi wa Iran wamekabiliana vilivyo na vita vya kiuchumi, kisiasa na kisaikolojia vya adui.

Rais Hassan Rouhani amesema hayo leo katika sherehe za usinduzi wa miradi 25 ya usambazaji umeme humu nchini na kusisitiza kuwa, si Wamarekani tu, bali hakuna mtu yeyote duniani aliyekuwa anatasawari kwamba wananchi wa Iran wangeliweza kusimama imara na kuilinda nchi yao katika mazingira haya magumu sana ya vita vya kila aina vya kiuchumi, kisiasa na kisaikolojia.

Amesema, vikwazo vya Marekani vimewaweka wananchi wa Iran katika hali nzito lakini pamoja na hayo na licha ya kuweko mashinikizo yote hayo, lakini kamwe wananchi wa Iran hawakukumbwa na upungufu wa maji, wala gesi, wala mafuta, wala chakula na wala kukatika umeme. Si hayo tu, lakini pia katika kipindi cha siku hizo kumeshuhudiwa mabadiliko makubwa nchini Iran katika nyuga za afya na matibabu, barabaa na reli na katika nyanja nyingine nyingi.

Rais Hassan Rouhani

 

Amesema, hata nchi zilizoendelea zaidi za Magharibi zimekumbwa na matatizo kutokana na wimbi la maambukizi ya kirusi cha corona, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na licha ya kuwa chini ya vikwazo vikubwa kupindukia, imepata mafanikio makubwa katika kupambana na ugonjwa wa COVID-19. 

Vile vile amesema, kila mwezi vijiji 35 vya Iran vinaunganishwa na gridi ya taifa ya umeme, asilimia 30 ya watu wasio na matumizi makubwa ya umeme wanasamehewa kulipa bili na hali hiyo karibuni hivi itajumuisha pia watumiaji sahihi wa gesi na maji kote nchini Iran.

Tags