Dec 04, 2020 12:09 UTC
  • Umoja wa Mataifa ulaani ugaidi Iran kama unavyolaani ugaidi Ufaransa, Austria

Katibu wa Ofisi ya Haki za Binadamu katika Idara ya Mahakama ya Iran amesema Umoja wa Mataifa unapaswa kulaani ugaidi unaojiri Iran sawa na unavyolaani ugaidi unaojiri Ufaransa na Austria, japo mara moja.

Ali Bagheri, Katibu wa Ofisi ya  Haki za Binadamu katika Idara ya Mahakama ya Iran ameyasema hayo katika barua alizotuma kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa kuhusu tukio la hivi karibuni la kuuawa kigaidi mwanasayansi bingwa wa nyuklia na sekta ya ulinzi nchini Iran, shahidi Mohsen Fakhrizadeh. Ameongeza kuwa, msimamo wa umoja wa mataifa wa kupuuza na kutochukua hatua za kivitendo kuhusu jinai hiyo ni sawa na kuhalalisha ugaidi na jambo hilo litachangia kuenea misimamo mikali na ugaidi duniani kote.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres

Katibu wa Ofisi ya  Haki za Binadamu katika Idara ya Mahakama Iran amekumbusha namna Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alivyochukua msimamo wa wazi kulaani ugaidi katika nchi zingine hasa matukio ya hivi karibuni ya hujuma za kigaidi Austria kupitia taarifa ya Novemba 3 2020 na Ufaransa kupitia taarifa ya  Septemba 17 2020. Baqeri amesema Iran inamtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alaani moja kwa moja na bila mapendeleo mauaji ya mwanasayansi wa nyuklia wa Iran na atambue jinai hiyo kuwa ni ugaidi.

Baqeri amesema ugaidi wa kiserikali unatumiwa na madola makubwa kufikia malengo haramu na yaliyo kinyume cha sheria. Amesema ugaidi wa kiserikali ni tishio kwa amani na usalama katika uga wa kimataifa.

Ikumbukwe kuwa, Profesa Mohsen Fakhrizadeh,  Mkuu wa Shirika la Utafiti na Ubunifu katika Wizara ya Ulinzi ya Iran ambaye pia alikuwa mwanasayansi bingwa katika sekta ya nyuklia ya Iran alipigwa risasi na kuuawa Ijumaa 27 katika hujuma ya kigaidi nje kidogo ya mji wa Tehran. Ushahidi wa awali umebaini kuwa ugaidi huo ulitekelezwa na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa ushirikiano na kundi la kigaidi la MKO.