Dec 04, 2020 12:18 UTC
  • Vikwazo dhidi ya Iran vimelenga dawa na bidhaa za tiba

Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amehutubu katika kikao cha ngazi za juu cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kukabiliana na janga la COVID-19 na kusema vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Iran vimezuia dawa na bidhaa zingine za tiba kuwafikia watu wa Iran.

Katika hotuba yake kwa njia ya video usiku wa kuamkia Ijumaa, Waziri wa Afya wa Iran Daktari Saeed Namaki amesema tokea mwanzo wa janga la COVID-19, Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na COVID-19 Iran chini ya uwenyekiti wa Rais Hassan Rouhani na uungaji mkono kikamilifu wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu imekuwa ikitumia uwezo wote wa kitaifa kukabiliana na COVID-19. Aidha amesema sera ya kamati hiyo imekuwa ni kusisitiza ushirikiano wa serikali na wananchi katika kufanikisha vita dhidi ya janga la COVID-19.

Amesema pamoja na kuwepo janga la COVID-19 Iran imeweza kuendeleza huduma zingine muhimu za afya kwa kinamama wajawazito, watoto na pia imeendeleza chanjo na pia wanaougua HIV na Kifua Kikuu au TB wanapata matibabu bila tatizo lolote.

Waziri wa Afya wa Iran Daktari Saeed Namaki

Hali kadhalika Daktari Namaki amesema pamoja na kuwepo vizingiti vilivyo kinyume cha sheria na vikwazo, serikali imetoa misaada maalumu ya kifedha kwa watu masikini na wasiojiweza katika jamii katika kipindi hiki cha janga la COVID-19.

Aidha amesema serikali imetekeleza hatua za kuwasaidia wafanyabiashara wadogowadogo waliopata hasara kutokana na janga la COVID-19. Waziri Namaki pia amesema serikali ya Iran inatoa huduma za bura za upimaji COVID-19 na matibabu kwa raia milioni 3.5 wanaoishi Iran kisheria na kinyume cha sheria bila kuwabagua.

Tags