Dec 14, 2020 04:50 UTC
  • Iran yalalamikia taarifa ya Ufaransa ya kumuunga mkono mhalifu aliyenyongwa

Iran imemuita balozi wa Ufaransa mjini Tehran Philippe Thiebaud kulalamikia taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo ya Ulaya ambayo imelaani kutekelezwa hukumu ya kunyongwa Ruhullah Zam, aliyepatikana na hatia ya kusimamia mtandao uliokuwa ukiendesha propaganda chafu dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Ulaya katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Jumapili alimuita balozi huyo wa Ufaransa na kumkabidhi malalamiko rasmi ya Iran kuhusu taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa.

Siku ya Jumamosi Ufaransa ilibainisha hasira zake baada ya kunyongwa Zam, ambaye kabla ya kukamatwa kwake alikuwa akiendesha propaganda zake dhidi ya Iran akiwa mjini Paris.

Siku ya Jumamosi, Ruhullah Zam, kinara wa mtandao wa habari wa Amad News ambao ulikuwa unaeneza propaganda dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu alinyongwa kufuatia hukumu iliyotolewa na mahakama.

Kwa miaka kadhaa, Zam alikuwa akitumiwa na mashirika ya kijasusi ya ajinabi pamoja na makundi ya wanaopinga Mapinduzi ya Kiislamu ambapo alisaidiwa kuanzisha mtandao wa habari wa Amad News nje ya Iran.

Ruhullah Zam akiwa mahakamani wakati wa kusikilizwa kesi yake

Mtandao huo wa habari ulikuwa ukieneza habari bandia na feki dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa lengo la kuvuruga usalama wa nchi.

Mamluki huyo alikamatwa mwezi Okotoba mwaka jana katika oparesheni maalumu ya Idara ya Intelijensia ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na kisha akafikishwa mahakamani ambapo alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifo kwa kutiwa kitanzi.

Zam alikamatwa katika oparesheni maalumu ambayo ilikuwa pigo kwa mashirika ya kijasusi ya nchi za Magharibi aliyokuwa akiyafanyia kazi hasa Ufaransa.

 

Tags