Dec 19, 2020 10:47 UTC
  • Haki za binadamu; chombo cha kisiasa cha Magharibi kwa ajili ya kuishinikiza Iran

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa kupitishwa azimio lililo dhidi ya Iran katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hakuna itibari yoyote ya kisheria na kwamba waliobuni azimio hilo wanazitumia vibaya taasisi za kimataifa.

Akizungumzia azimio hilo ambalo liliwasilishwa katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Canada kwa uungaji mkono wa nchi za Ulaya na utawala haramu wa Israel, Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amaesema kuwa, hatua ya serikali ya Canada na wangine waliobuni azimio hilo ni mfano wa wazi kuhusu namna watu wanavyotumia vibaya maana na thamani za haki za binadamu kwa ajili ya kufikia malengo yao ya muda mfupi ya kisiasa, na hilo ni jambo linalopaswa kulaaniwa.

Azimio hilo lililo dhidi ya Iran na ambalo kama tulivyotangulia kusema liliwasilishwa na Canada lilipitishwa kwa kura 80 katika Baraza Kuu la Usalama na kupingwa na karibu nchi nyingine 115 wanachama wa Umoja wa Mataifa, suala linalothibitisha wazi kwamba nchi nyingi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinapinga undumakuwili unaofanywa na baadhi ya nchi kuhusu suala zima la haki za binadamu.

Saeed Khatibzadeh

Undumakuwili huo kuhusu haki za binadamu daima umekuwa ukitekelezwa dhidi ya Iran. Mashinikizo yanaendelea kutolewa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kisingizio cha kutetea haki za binadamu katika hali ambayo vikwazo vya kiuchumi, vikwazo vya dawa na kuuawa kigaidi maafisa wa ngazi za juu wa Iran ni ukiukaji wa wazi wa haki hizo za binadamu lakini nchi zote za Ulaya zimekaa kimya na kukataa kuzungumzia ukiukaji huo ulio dhahiri.

Rekodi na historia ya waliowasilisha muswada huo katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, imejaa matukio ya kuaibisha kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu na hasa kupitia uingiliaji wa kijeshi katika nchi nyingine na vile vile mauzo ya silaha kwa baadhi ya tawala kandamizi za Kiarabu katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).

Kimya cha nchi za Magharibi mbele ya ukiukaji wa haki za binadamu nchini Yemen, kuuziwa silaha baadhi ya nchi za Kiarabu ambazo hatimaye huzitumia kwa ajili ya kuua kinyama watu wasio na hatia huko Yemen na hasa wanawake na watoto, ni mfano wa wazi wa undumakuwili unaofanywa na nchi za Magharibi kuhusu suala la haki za binadamu.

Uchunguzi wa historia ya nchi za Magharibi kuhusu haki za binadamu unathibitisha wazi kwamba nchi za Ulaya na Marekani hutumia kisingizio cha haki za binadamu na kutoa mashinikizo dhidi ya nchi pinzani na zisizokubali siasa zao za kibeberu pale zinapoona kwamba maslahi yao yamo hatarini.

Namna watu wa Yemen wanavyodhalilishwa na wanaodai kutetea haki za binadamu

Hatua hiyo mbovu na ya kusikitisha ya nchi za Magharibi haisaidii lolote katika kuimarisha hali ya haki za binadamu ulimwenguni bali huendeleza tu siasa za nchi hizo katika kutoa mashinikizo dhidi ya nchi huru na zinazojitawala.

Katika uwanja huo, Ali Baqer Kani, Katibu wa Idara ya Haki za Binadamu ya Iran ameashiria undumakuwili unaofanywa na nchi za Magharibi kuhusu suala zima la haki za binadamu na kusema: Fikra ya kwanza ni ya Wamagharibi ambao wanaliona suala la haki za binadamu kuwa linapasa kulinda maslahi na siasa zao na fikra ya pili ni ya Iran ambayo siasa zake zimejengeka katika msingi wa kuheshimu haki za binadamu.

Haki za binadamu ni moja ya vyombo vinavyotumiwa vibaya na watawala wa Magharibi kufikia malengo yao, hivyo azimio lililopasishwa katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa pendekezo la Canada na kwa ushirikiano wa Marekani na utawala haramu wa Israel ni muendelezo ule ule wa kutoa mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ili kufikia malengo yao haramu.

Tags