Jan 05, 2021 12:31 UTC

Kamanda wa kikosi cha nchi kavu cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kikosi hicho kimepata mafanikio makubwa na ya kipekee katika uzalishaji na utumiaji wa droni yaani ndege zisizo na rubani.

Kwa mujibu wa shirika la Iran Press, Brigedia Jenerali Kioumars Heydari amesema hayo leo Jumanne, pambizoni mwa mazoezi ya ndege zisizo na rubani za kikosi cha nchi kavu cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu yanayoendelea huko Semnan, kaskazini mwa Iran na kusisitiza kuwa, droni ni silaha muhimu sana katika medani za vita na kwamba Iran imepata mafanikio ya aina yake na ya kipekee katika uzalishaji na utumiaji wa ndege hizo zisizo na rubani.

Kamanda huyo wa kikosi cha nchi kavu cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vile vile ametoa ufafanuzi wa droni za kila namna zinazoshiriki kwenye mazoezi hayo ya kivita na kusema kwamba kikosi cha nchi kavu cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu kina nguvu kubwa za ndege za aina hiyo.

Baadhi ya droni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Mazoezi makubwa ya kwanza ya droni za Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu yameanza leo Jumanne katika mkoa wa Semnan wa kaskazini mwa Iran yakishirikisha mamia ya ndege hizo zisizo na rubani.

Kwa upande wake, Admirali Sayyid Mahmoud Mousavi, naibu wa operesheni wa mkuu wa jeshi la Jamhuri ya Kiislamu amesema kuwa, mazoezi makubwa ya kijeshi ya ndege zisizo na rubani za Iran yanafanyika katika mazingira yenyewe ya kivita yakishirikisha vikosi vya nchi kavu, vikosi vya ulinzi wa anga na rada, vikosi vya majini na angani vya jeshi la Iran na inabidi droni hizo ziendeshe operesheni zake kwa njia bora kabisa.