Jan 09, 2021 13:01 UTC
  • Rouhani: Wananchi wa Iran hawawi wenzo wa kufanyia majaribio ya chanjo za nchi za kigeni

Rais Hassan Rouhani amesema, wananchi wa Iran hawatakuwa wenzo wa kufanyia majaribio chanjo za nchi za kigeni.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo mjini Tehran katika kikao cha 51 cha tume ya taifa ya kupambana na corona na akabainisha kwamba, mashirika ya kigeni yalitaka kuipatia Iran aina kadhaa za chanjo ili zifanyiwe majaribio kwa watu, lakini wizara ya afya, tiba na mafunzo ya utabibu ikazuia suala hilo.

Rais Rouhani ameashiria baadhi ya uvumi unaoenezwa kuhusu kununuliwa chanjo ya corona na akasema: inapasa redio na televisheni ya taifa pamoja na vyombo vingine vya habari vikabiliane na uenezaji uvumi kama huo; na kwa upande mwingine, wananchi wanatakiwa wasikilize maneno ya wataalamu wa wizara ya afya na kutohadaiwa na watu wenye nia mbaya.

Wananchi wa Iran wakipigwa chanjo ya majaribio ya corona iliyotengenezwa nchini ya COVIRAN Barekat

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kwamba, kuandaa na kununua chanjo ya corona ni katika vipaumbele vya serikali; na akasisitiza kuwa, kupiga chanjo hakumaanishi kwamba miongozo ya kiafya isiendelee kuzingatiwa na kufuatwa.

Rais Rouhani amesema, ikiwa athari ya chanjo ya corona itakuwa ni ya asilimia mia moja, hali ambayo haipatikani kwa chanjo yoyote ile, utahitajika muda wa wiki kadhaa mpaka kuonekana athari zake.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, takriban ulimwengu mzima inashauriwa kwamba, hata kama kutakuwepo na chanjo za kutosha kwa ajili ya watu wote, kutakuwa na haja ya kuendelea kuchunga miongozo ya kiafya kwa muda usiopungua miezi mingine mitano hadi sita, kwa hivyo wananchi wa Iran pia wanapaswa waendelee kuchunga miongozo ya kiafya.../

Tags