Jan 12, 2021 05:06 UTC
  • Iran yataka Polisi ya Kimataifa (Interpol) iwakamate wauaji wa mashahidi Soleimani, Fakhrizadeh

Msemaji wa Polisi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, Iran imeikabidhi Polisi ya Kimataifa, Interpol, taarifa kuhusu watu wanne waliohusika katika mauaji ya mwanasayansi wa nyuklia wa Iran shahidi Mohsen Fakhrizadeh na pia watu wengine waliohusika katika mauaji ya shahidi Qassem Soleimani."

Brigedia Jenerali Mahdi Hajian ameyasema hayo Jumatatu mjini Tehran na kusema Iran imeitaka Interpol itangaza notisi nyekundu kwa ajili ya kukamatwa watu wanne waliomuua shahidi Fakhrizadeh na pia  itoe notisi nyekundu kwa wahusika wa mauaji ya shahidi Soleimani. Ameongeza kuwa, katika kipindi cha miezi tisa iliyopita ya mwaka wa Kiirani, watu 37 waliokuwa wanaswka na vyombo vya usalama vya Iran wamerejeshwa nchini kutoka maeneo mbali mbali duniani. 

Wakati huo huo, familia za wanasayansi wa nyuklia ambao wameuawa shahidi zimewasilisha mashtaka dhidi ya serikali ya Marekani kutokana na kuwa inaunga mkono vitendo vya kigaidi vya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Wakili wa familia hizo, Afzali Nikoo, amesema serikali ya Iran pia itafuatilia kadhia hiyo katika uga wa kimataifa. Amesema familia hizo zimewasilisha mashtaka dhidi ya watu 32 katika serikali ya Marekani na zinataka fidia ya dola milioni 100.

Ikumbukwe kuwa, Magaidi wenye silaha siku ya Ijumaa ya tarehe 27 Novemba mwaka 2020 waliishambulia gari iliyokuwa imembeba Mohsen Fakhrizadeh, Mkuu wa Shirika la Utafiti na Ubunifu la Wizara ya Ulinzi ya Iran na kumuua shahidi mwanasayansi huyo mkubwa wa nyuklia na masuala ya ulinzi. 

Maafisa wa Iran wamesema utawala wa Kizayuni wa Israel ulihusika katika mauaji ya mwanasayansi huyo wa nyuklia.

Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) alielekea Iraq Januari 3 mwaka 2020 kufuatia mwaliko rasmi wa wakuu wa Iraq.

Punde baada ya kuwasili Iraq aliuawa shahidi katika hujuma ya ndege za kivita za jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad. Aidha katika hujuma hiyo ya kigaidi Abu Mahdi Al Muhandis, Naibu Mkuu wa Harakati ya Kujitolea ya Wananchi wa Iraq, naye pia aliuawa shahidi akiwa ameandamana na Qassem Soleimani. Watu wengine wanane waliokuwa katika msafara huo nao pia waliuawa shahidi.

 

Tags