Jan 14, 2021 13:24 UTC
  • Rouhani: Ongezeko la wawekezaji wa kigeni Iran ni ishara ya kufeli vikwazo vya Marekani

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema ongezeko la asilimia 56 ya wawekezaji wa kigeni katika maeneo ya biashara huru nchini Iran ni ishara ya kufeli sera za Marekani za ugaidi wa kiuchumi na mashinikizo ya juu kabisa.

Rais Rouhani ameyasema hayo leo Alhamisi wakati wa kuzinduliwa miradi 60 ya miundo msingi katika maeneo ya biashara huru kote Iran.

Akizungumza kwa njia ya video katika uzinduzi huo, Rais Rouhani amesema takwimu zinaonyesha kuwa, Iran imefanikiwa katika kuyabadilisha maeneo hayo huru ya biashara kutoka kuwa vituo vya kuagiza bidhaa kutoka nje na badala yake kuwa vituo vya kuuza bidhaa katika soko la kimataifa.

Rais Rouhani amesema maeneo hayo huru yametumika kuuza nje bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 138 huku Iran ikitumia maeneo hayo kuagiza kutoka nje bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 47.

Bandari nchini Iran

Aidha amesema maeneo hayo huru ya kiuchumi yanaweza kusaidia uchumi wa Iran kukabiliana na vikwazo. Ameongeza kuwa, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kumeshuhudiwa ongezeko la asilimia 56 la wawekezaji wa kigeni na wa ndani ya nchi katika maeneo hayo huru ya kibiashara. Rais amebaini kuwa ongezeko hilo linaonyesha mafanikio ya sera za serikali katika maeneo hayo.

Rais Rouhani amesema maeneo mengi ya bishara huru yaliyoko kaskazini na kusini mwa Iran pia yanaweza kuwa vivutio vya kitalii.

Tags