Jan 16, 2021 11:09 UTC
  • Maneva ya 15 ya Mtume Mtukufu (SAW); dhihirisho la nguvu ya makombora na ndege zisizo na rubani

Vitisho vya kijeshi na kuibua machafuko vilikuwa moja ya machaguo ya kimkakati ya maadui kwa ajili ya kuuangusha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu tangu mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu.

Vitisho hivyo viliongezeka na kuingia katika hatua mpya baada ya Iran kupita salama na kuweka nyuma vita vya kulazimishwa na kushindwa maadui katika vita hivyo vya miaka 8 vya kujitetea kutakatifu. Muda si mrefu, vikwazo vya silaha vya muda mrefu vilianza kutekelezwa dhidi ya Iran kwa lengo la kuidhoofisha kijeshi na hivyo kuiweka katika hatari ya kushambuliwa na maadui wakati wowote.

Ni wazi kuwa katika kukabiliana na siasa hizo za maadu, Iran haikuwa na chaguo jingine la kuweza kulinda usalama wa nchi ila kutegemea suhula na uwezo wa ndani na kujiimarisha kijeshi zaidi mkabala na vitisho.

Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Amiri Jeshi Mkuu katika sehemu moja ya hotuba yake kwa mnasaba wa maadhimisho ya mapambano ya kihistoria ya wananchi wa mji wa Qum ya tarehe 19 mwezi Dei mwaka 58 Hijria Shamsiya alisisitiza juu ya umuhimu wa uwezo wa kiulinzi na akakumbushia historia chungu ya kushindwa nchi hii kukabiliana na mashambulizi ya anga ya Saddam na kueleza kuwa: Iran wakati huo haikuwa na uwezo wa kukabiliana na makombora yaliyokuwa yakivurumishwa katika mji wa Tehran na katika miji mingine mbalimbali ya Iran; na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikupasa kuiacha nchi katika hali hiyo bila ya kuchukua hatua yoyote.  

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei  

Kwa msingi huo,  moja ya sehemu nyeti na muhimu ya kiulinzi ya Iran ni kuwa na uwezo wa ulinzi wa makombora ambao ni muhimu katika upande wa kimkakati na kistratejia katika kuzuia mashambulizi na hujuma ya maadui. 

Sehemu ya uwezo huu wa kiulinzi wa Iran katika sekta ya makombora ulidhihirishwa Ijumaa tarehe 15 mwezi huu katika marhala ya kwanza ya maneva ya 15 ya Mtume Mtukufu (SAW) kwa kutekelezwa oparesheni za ubunifu za makombora na ndege zisizo na rubani (droni) za kikosi cha anga cha jeshi la Sepah. 

Maneva ya 15 ya Mtume Mtukufu (SAW)

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Meja Jenerali Hossein Salami amesema pambizoni mwa maneva hiyo kuwa: Ujumbe wa mazoezi haya ni uwezo na irada ya dhati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kulinda mamlaka ya nchi, kulinda mfumo mtukufu wa Jamhuri ya Kiislamu na thamani zake mbele ya maadui wa Uislamu na Iran. 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imechukua hatua kubwa ili kujidhaminia uwezo wa kukabiliana na mashambulizi ya kijeshi dhidi yake kupitia mchakato wa ujuzi na teknolojia ya kubuni na kutengeneza makombora ya balistiki ndani ya nchi. 

Kwa mtazamo huo,  uwezo wa makombora wa Iran unahesabiwa kuwa nguzo ya kukabiliana na mashambulizi yoyote dhidi yake. Jarida linalochapishwa nchini Marekani la  National Interest limetoa tathmini yake kuhusu uwezo wa makombora wa Iran na kukiri juu ya nukta hii kuwa: Iran imevuruga mlingano uliokuwepo mkabala na uwezo wa kijeshi wa Marekani na waitifaki wake katika eneo. Tunaweza kusema bayana kuwa mlingano wa kistratejia hivi sasa umebadilika kwa maslahi ya Iran. 

Ndio maana Marekani, Ulaya na washirika wao katika eneo wakafanya kila wanaloweza kuiweka Iran chini ya mashinikizo makubwa ili kupunguza uwezo wake wa makombora. Pande hizo aidha zimefanya kila zinaloweza kukiuka mapatano ya JCPOA na hivyo kuibua anga mpya ili kuirejesha kadhia ya uwezo wa makombora wa Iran katika meza ya mazungumzo; lengo ambalo katu halitatimia kwa hali yoyote ile.   

Uwezo wa makombora wa Iran ni dhihirisho la nguvu na uwezo wake wa kijeshi na kiulinzi katika kukabiliana na adui. Kama alivyosisitiza Jenerali Amir-Ali Hajizadeh Kamanda wa Kikosi cha Anga cha IRGC pambizoni mwa  marhala ya awali ya meneva ya 15 ya Mtume Mtukufu (SAW): Nguvu mpya imezaliwa ndani ya kikosi hiki katika marhala ya awali  ya maneva ya 15 ya Mtume Mtukufu (SAW) kwa kuunganisha uwezo mpya wa makombora na oparesheni za droni na kwa kustafidi na teknolojia ya akili bandia.  

Jenerali Amir-Ali Hajizadeh, Kamanda wa Kikosi cha Anga cha IRGC

Umuhimu wa kiwango hiki cha uwezo wa kijeshi ambao ni matokeo ya tafiti na hatua za ustawi katika sekta ya ulinzi  ya Iran kwa hakika una nafasi muhimu katika mahesabu ya adui.