Jan 17, 2021 02:22 UTC
  • Salami: Makombora ya balestiki ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya kiulinzi ya Iran

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema, utumiaji wa makombora ya balestiki ambayo yana uwezo ya kulenga shabaha zilizokusudiwa zikiwa baharini ni mafanikio makubwa ya kiulinzi kwa Iran.

Meja Jenerali Hussein Salami ameyasema hayo Jumamosi pembeni ya awamu ya mwisho ya manuva ya 15 ya IRGC yaliyopewa jina la Mtume Mtukufu SAW yanayofanyika katika eneo la umma la jangwani katikati ya Iran.

Meja Jenerali Salami ameashiria malengo ya kufanyika awamu hiyo ya mazoezi ya kijeshi na akaeleza kwamba, "moja ya malengo muhimu kwetu katika sera na stratejia za kiulinzi ni kuwa na uwezo wa kuzilenga manowari za adui, zikiwemo manowari za kubebea ndege za kivita na manowari za vita kwa kutumia makombora ya balestiki ya masafa ya mbali."

Mazoezi ya kijeshi ya IRGC

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza kwamba, ilivyozoeleka ni kuwa vilengwa vitembeavyo baharini hutunguliwa kwa kutumia makombora ya kruzi yaendayo kwa kasi ndogo, lakini kuweza kutungua vilengwa vitembevayo baharini vilivyoko kwenye vina vikubwa na katika masafa ya mbali kutoka aradhi ya Iran kwa kutumia makombora ya balestiki ni mafanikio makubwa ya kiulinzi ambayo kikosi cha anga za mbali cha SEPAH kimeweza kuyafikia kwa ukamilifu.

Kamanda Salami amesisitiza kuwa, "leo tumeshuhudia ufanyaji mazoezi ya kiwango cha juu kiuwezo ya kikosi cha anga za mbali cha Sepah; na hiyo ni sehemu ya sera za ulinzi zinazofanyiwa tathimini katika medani za mazoezi ya kijeshi ili ziweze kutekelezwa katika mazingira ya uhalisia pale itakapohitajika".../

 

Tags