Jan 18, 2021 04:49 UTC
  • Iran yaitahadharisha Marekani kuhusu ndege za kivita aina ya B-52

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif ameashiria uwepo wa ndege za kivita za Marekani aina ya B-52 katika eneo la Asia Magharibi na kuonya kuwa, Iran haitasita kutungua chombo chochote kinachokiuka anga yake.

Katika ujumbe alioutuma katika ukurasa wake wa Twitter Jumapili, Zarif  amesisitiza kuwa, Iran si nchi chokozi na kuongeza kuwa, 'katika kipindi cha miaka 200, Iran haijawhi kuanzisha vita.'

Hata hivyo Zarif amesema Iran haitishiki na  itatoa jibu kali kwa wavamizi. Hali kadhalika Zarif amemshauri rais Donald Trump wa Marekani anayeondoka madarakani kutopoteza pesa za walipa kodi wa Marekani kwa harakati zisizo na maana. Zarif ameandika: "Unapaswa kutumia mabilioni ya fedha za walipa kodi katika masuala ya afya yao." Zarif hapo alikuwa akiashiria hali mbaya ya maambukizi ya corona nchini Marekani ambapo hadi sasa watu karibu laki nne wamepoteza maisha.

Ujumbe huo wa Twitter wa Zarif umekuja masaa kadhaa baada ya Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani kutangaza kuwa siku ya Jumapili ndege za kivita za B-52 zilizunguka eneo la Asia Magharibi au Mashariki ya Kati ikiwa ni mara ya pili kufanya hivyo mwaka huu wa 2021. Ndege hizo za B-52 zina uwezo wa kusheheni mabomu ya nyuklia.

Kamanda wa Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani , Jenerali Frank McKenzie amethibitisha kuwa ndege hizo zimeruka katika eneo.

Kombora la Iran likivurumishwa katika mazoezi ya kijeshi

Wiki iliyopita, Marekani na Saudi Arabia zilifanya mazoezi ya pamoja ya kivita baada ya mazoezi mengine kama hayo Disemba mwaka jana. Katika kujibu chokochoko hizo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Jumatano na Alhamisi lilifanya mazoezi makubwa ya kijeshi ya siku mbili yaliyopewa jina la Mtume Mtukufu SAW 15 ambapo kulifanyika majaribio ya makombora ya balistiki na ndege za kivita zisizo na rubani. Baadhi ya makombora yaliyofanyiwa majaribio katika mazoezi hayo yaliruka umbali wa kilomita 1,800 na kulenga manowari bandia za adui. Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Iran Meja Jenerali Baqeri amesema mazoezi hayo ni dalili ya wazi kuwa, iwapo maadui wa Jamhuri ya Kiislamu wana nia mbaya basi watashambuliwa kwa makombora na wataangamizwa. Siku ya mazoezi hayo, Shirika la Habari la Fox News liliripoti kuwa makombora ya masafa marefu yaliyorushwa kutoka Iran yalitua katika eneo lenye umbali wa maili 100 tu kutoka meli ya kivita ya Marekani ya Nimitz yenye uwezo wa kusheheni ndege.

Tags