Jan 18, 2021 14:28 UTC
  • Jenerali Baqeri: Marekani inaogopa uwezo wa kiulinzi wa Iran

Kamanda wa Vikosi vya Ulinzi vya Iran amesema harakati na mienendo ya Marekani katika eneo la Asia Magharibi haina thamani yoyote ya kioperesheni, na badala yake inaonesha wazi namna dola hilo la kibeberu linatiwa kiwewe na uwezo mkubwa wa kujihami wa Jamhuri ya Kiislamu.

Brigedia Jenerali Mohammad Baqeri ameashiria kuhusu uwepo wa ndege za kivita za Marekani aina ya B-52 katika eneo la Asia Magharibi na kueleza bayana kuwa: Katika hali ambayo Vikosi vya Ulinzi vya Iran vinafahamu kuwa maadui hawawezi kuchukua hatua yoyote kutokana na uwezo wa kiulinzi wa Iran, lakini vipo macho na vimejiandaa kikamilifu kujibu chokochoko zozote za adui.

Baqeri amesema hayo leo Jumatatu na kueleza bayana kuwa, katika kipindi cha siku 20 zilizopita, Majeshi ya Iran yamedhihirisha utayarifu wa taifa hili katika kulinda mamlaka na maslahi yake, kwa kufanyia majaribio kwa mafanikio makombora ya belestiki ya kutoka ardhini hadi angani.

Mapema jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif aliashiria kuhusu uchokozi huo wa Marekani na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu haitasita kutungua chombo chochote kinachokiuka anga yake.

Chokochoko za US katika eneo la Asia Magharibi

Zarif alisema hayo masaa machache baada ya Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani kutangaza kuwa ndege za kivita za B-52 zilizunguka eneo la Asia Magharibi, ikiwa ni mara ya pili kufanya hivyo mwaka huu wa 2021. Ndege hizo za B-52 zina uwezo wa kusheheni mabomu ya nyuklia.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza kuwa, Marekani itakabiliwa na jibu kali iwapo itachua hatua ya kutaka kuteteresha usalama wa nchi hii.

Tags