Jan 19, 2021 10:39 UTC
  • Tehran mwenyeji wa mkutano kwa njia ya video wa mabunge yanayounga mkono Quds na Palestina

Jumatatu ya jana tarehe 18 Januari, mji mkuu wa Iran Tehran ulikuwa mwenyeji wa mkutano uliofanyika kwa njia ya mawasiliano ya intaneti chini ya anuani ya "Gaza; nembo ya muqawama" wa mabunge yanayoiunga mkono Quds na Palestina.

Maspika na wawakilishi wa Mabunge kutoka Uturuki, Indonesia, Yemen, Pakistan, Algeria, Afghanistan, Qatar, Tunisia, Lebanon, Bolivia, Venezuela, Iraq, Syria, Afrika Kusini na Palestina walishikiri katika mkutano huo.

Kufanyika mkutano huo katika wakati huu kuna umuhimu wa pande kadhaa.

Umuhimu wa kwanza; mkutano huu ni ufuatiliaji wa suala la Palestina ikiwa kadhia muhimu zaidi katika Ulimwengu wa Kiislamu, suala ambalo linafuatiliwa na mabunge ya  nchi za Kiislamu yakiwa wawakilishi wa mataifa ya Kiislamu.

Umuhimu wa pili wa mkutano huu ni upande wa kimataifa wa kadhia ya Palestina. Mkutano huu umefanyika katika hali ambayo, jinai za utawala wa kigaidi wa Israel zimeingia katika hatua mpya kutokana na utumiaji mbaya wa utawala huo wa mazingira ya yanayotawala hivi sasa katika eneo na uga wa kimataifa. Utawala vamizi wa Israel ukipata himaya na uungaji mkono wa Marekani na katika pazia la mpango wenye njama wa 'Muamala wa Karne' umo mbioni kutekeleza mipango yake michafu ya kikoloni ya kuligawa eneo la Asia Magharibi.

Maandamano ya wananchi wa Palestina huko Baitul-Muqaddas

 

Filihali, licha ya kuweko maazimio lukuki ya Umoja wa Mataifa na kutambuliwa rasmi haki ya taifa la Palestina katika asasi za kimataifa ya kuwa na dola lake huru mji mkuu wake ukiwa Baitul-Muqaddas, lakini Israel ikiungwa mkono na Marekani inajiona kuwa iko juu ya sheria ambapo kwa kutenda aina kwa aina ya jinai za kivita na kutwisha matakwa yake, imepuuza kabisa maamuzi na maazimio ya asasi za kimataifa na hivyo kuhatarisha kabisa amani na uthabiti wa kimataifa.

Mwenendo huu maana yake ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa dunia, ambapo jamii ya kimataifa inapaswa kujitokeza na kukabiliana na ufidhuli huu wa Israel na kuonyeshha azma na irada yake ya kukataa uvamizi na dhulma dhidi ya taifa la Palestina.

Katika uwanja huo, Abdul-Amir Ruwaih, mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema: Kujikomba na kujikurubisha mataifa ya Kiarabu kwa utawala dhalimu wa Israel na kutia saini makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo kulikofanywa na baadhi ya viongozi wa mataifa ya Kiislamu kama Imarati, Bahrain na Sudan kwa usimamizi wa Marekani kutakuwa na taathira mbaya mno kwa kadhia ya Palestina na mapambano ya wananchi wa taifa hilo madhulumu dhidi ya Wazayuni maghasibu. Hatua ya mataifa hayo ya Kiarabu ya kujidhalilisha mbele ya siasa za serikali ya Marekani imeupa kiburi utawala vamizi wa Israel cha kuendeleza mipango yake ya kujitanua na kuandaa uwanja wa kufanya hujuma kila leo na kupuuza kabisa haki za wananchi wasio na ulinzi wa Palestina.

 

Maandamano ya kupinga kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel

Upande wa tatu wa umuhimu wa kufanyika mkutano huu kuhusu Palestina, ni kuakisi uhakika wa mambo wa kadhia ya Palestina na udharura wa kuzingatia matokeo ya jinai za Israel katika eneo na ulimwenguni kwa ujumla.

Fikra za waliowengi ulimwenguni hususan baada ya kuibuka na kusambaa virusi vya corona  na kushuhudia ukatili na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel jinsi utawala huo unavyoamiliana na watu milioni mbili wanaokabiliwa na mzingiro wakiwemo wanawake na watoto huko katika Ukanda wa Gaza na hatua yake ya kuzuia kuwafikia misaada ya kibinadamu kama ya chakula na dawa, zimefikia natija hii kwamba, utawala wa kigaidi wa Israel wenye kumiliki silaha za nyuklia na za kemikali ndio tishio na hatari kubwa zaidi kwa jamii ya mwanadamu, amani na usalama wa kimataifa.

Katika mazingira haya hasasi na nyeti, kuweko fikra na mitazamo mimoja  ya Mabunge ya Kiislamu, bila shaka ni fursa kwa ajili ya kukumbusha ukweli huu na kusisitiza juu ya udharura wa kuunga mkono haki za mataifa yanayokandamizwa na kudhulumiwa hususan taifa la Palestina na kuikomboa Quds kutoka katika makucha ya Uzayuni wa Kimataifa.

Wanamambano wa Hamas katika Uukanda wa Gaza

 

Hapana shaka kuwa, utawala bandia wa Israel na Uzayuni hauna nafasi kabisa katika mustakabali wa Asia Magharibi. Hivi sasa kuna ishara za wazi za kuporomoka Marekani na kuondoka majeshi ya kigeni katika eneo ni jambo ambalo limedhihirika bayana.

Ardhi za Palestina na Quds zinazokaliwa kwa mabavu, hapana shaka iko siku zitakombolewa na hatimaye wakimbizi wa Kipalestina kurejea katika ardhi za mababu zao; kwani kizazi cha leo cha Palestina kina umaizi na utambuzi wa wazi kuhusu utambulisho wa ardhi zao, na harakati ya muqawama imeazimia kwa dhati na kwa nguvu zote kurejesha haki zote za taifa la Palestina zilizoporwa na kughusubiwa na maadui Wazayuni.