Jan 20, 2021 12:19 UTC
  • Rouhani: Washington imegeuzwa kuwa kambi ya kijeshi katika siku ya kuapishwa Biden

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa leo ni siku ya kufikia ukomo wa utawala wa Donald Trump na kueleza kuwa Washington imgeuzwa kuwa kambi ya kijeshi katika siku ya kuapishwa rais mpya wa Marekani.

Akizungumza leo katika kikao cha baraza la mawaziri, Rais Hassan Rouhani amekutaja kutengwa kisiasa Marekani kuwa ni urithi alioubakisha Trump na kuongeza kuwa, hii leo Marekani imesalia peke yake katika taasisi za kimataifa, katika kadhia ya Palestina, mapatano ya JCPOA na masuala mengine ya kimataifa kutokana na sera mbovu za Trump katika siasa za nje za nchi hiyo. 

Mapatano ya kimataifa ya JCPOA yaliyopasishwa na Baraza la Usalama la UN  

Rais Rouhani ameeleza kuwa, jamii ya Marekani kugawanyika katika kambi mbili ni matunda ya urithi wa Trump na kueleza kuwa, katika kipindi chote cha uongozi wake wa miaka minne Trump hajakuwa na mafanikio yoyote ghairi ya kutenda dhulma, ufisadi na kuwasababishia matatizo na masaibu mbalimbali wananchi wake na ulimwengu mzima. 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia ugaidi wa kiserikali wa Marekanii na kueleza kuwa: Rais huyo wa Marekani alitamka wazi kwamba amemuua kamanda mmoja wa kijeshi wa ngazi ya juu ambaye alikuwa ziarani katika nchi fulani. Rais Rouhani amesema kuwa, kwa kutekeleza mauaji hayo Marekani imedhihirisha namna ilivyo mhimili wa ugaidi wa kiserikali duniani. 

Akiendelea na hotuba yake mbele ya kikao cha baraza la mawaziri, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, taifa la Iran na nchi nyingine za dunia zimebainikiwa ukweli huu kwamba, siasa za ugaidi wa kiuchumi na mashinikizo ya kiwango cha juu zimegonga mwamba kwa asilimia mia moja; na wananchi wa Iran hawajatoa mwanya kwa maadui kufikia malengo yao kutokana na muqawama na kusimama kwao imara.