Jan 21, 2021 03:10 UTC
  • Biden
    Biden

Sherehe za kutawazwa Joseph Robinette Biden Jr. kuwa rais wa 46 wa Marekani zimefanyika katika hali ambayo, Jumanne, tarehe 19 Januari 2021, maafisa wa ngazi za juu wa serikali yake walitumia kikao cha Baraza la Sanate la nchi hiyo kutangaza misimamo yao kuhusu Tehran na masuala yanayohusiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Antony Blinken, waziri wa mambo ya nje mtarajiwa wa Marekani alisisitiza kuwa, serikali ya Biden itaendelea na msimamo wake wa kuhakikisha Iran haimiliki kile alichodai silaha za nyuklia na wakati huo huo lakini alikiri kwamba makubaliano ya nyukli aya JCPOA yamefanikiwa kudhibiti shughuli za nyuklia za Iran hata hivyo kujitoa Marekani katika makubaliano hayo ya kimataifa kumeiandalia Iran fursa ya kuongeza kiwango chake cha kurutubisha urani.

Naye Avril Haines ambaye anatarajiwa kuwa mkuu wa kusimamia masuala ya kijasusi ya kitaifa ya Marekani katika serikali ya Biden amesema, kama Iran itarejea kuheshimu kikamilifu mapatano ya nyuklia ya JCPOA, basi Marekani nayo itarejea. Hata hivyo amesema hivi sasa jambo hilo inaonekana liko mbali  na kuna masafa marefu hadi kufikia huko. Ameongeza kuwa, kurejea Marekani kwenye mapatano ya nyuklia ya Iran lazima kujumuishe pia mazungumzo kuhusu nguvu za makombora za Iran na shughuli za Tehran alizodai ni za kuzusha machafuko katika eneo hili.

Bunge la Iran limepasisha muswada wa kuiwajibisha Iran kurutubisha urani kwa asilimia 20

 

Misimamo hiyo ya maafisa wa serikali ya Joe Biden inaonesha wazi kwamba, tofauti na walivyodhani baadhi ya watu kwamba Marekani itabadilisha haraka siasa zake kuhusu Iran hususan suala la mapatano ya nyuklia ya JCPOA, ukweli wa mambo ni hii misimamo inayotangazwa sasa hivi na maafisa wa serikali ya Biden ambayo kimsingi ni misamiati ile ile ya kila siku ya Marekani kuhusu Iran.

Amma kukumbushia suala hili pia ni jambo muhimu kwamba, hata serikali ya Donald Trump ilitumia visingizio mbalimbali kuhalalisha kujitoa kwake kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA mwezi Mei 2018. Trump aliiwekea Iran vikwazo vikubwa ambavyo havijawahi kuwekewa nchi yoyote ile katika historia, kwa ndoto kwamba angeliweza kuilazimisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran isalimu amri na iipigie magoti Marekani. Hata hivyo na licha ya propaganda nyingi za kujaribu kuonesha kuwa vikwazo hivyo vya kiwango cha juu mno vya Marekani dhidi ya Iran eti vimefanikiwa, lakini ukweli ni kwamba halijafanikiwa hata moja kati ya mambo 12 yaliyotajwa na Mike Pompeo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani kuhusu malengo ya vikwazo hivyo. 

Paul Pillar, mtalamu wa masuala ya kisiasa wa Marekani anasema, vita vya kiuchumi na mashinikizo ya kiwango cha juu mno ya Trump dhidi ya Iran si tu hayakuinufaisha chochote Marekani, lakini pia yameshindwa katika kila kona.

Baadhi ya pande zilizobakia ndani ya JCPOA baada ya Marekani kujitoa

 

Labda mpenzi msikilizaji utajiuliza, ni nini sababu ya kushindwa vikwazo hivyo vya Marekani mbele ya Iran? Majibu ni wazi kwamba muqawama wa kiwango cha juu wa Iran na kusimama kwake kidete kukabiliana na vikwazo hivyo, ndiyo sababu ya kufeli mashinikizo hayo ya kiwango cha juu mno ya Marekani. Wakati huo huo kutokana na nchi za Ulaya zilizobakia ndani ya makubaliano ya JCPOA kushindwa kutekeleza ahadi zao, Tehran nayo iliamua kupunguza ahadi zake ndani ya mapatano hayo kwa awamu 5. Hivi sasa pia, na baada ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) kupasisha muswada wa kuiwajibisha Iran irutubishe urani kwa kiwango cha asilimia 20, akiba ya urani iliyorutubishwa nchini Iran inaongezeka siku baada ya siku. Jambo hilo linaonesha wazi kwamba Iran haitanii wakati inaposema itachukua hatua fulani ya kulinda manufaa yake ya kitaifa. Tena hatua hizo zinafanyika kisheria na hata Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA ambao ndio unaosimamia makubaliano ya JCPOA umesisitiza mara chungu nzima kuwa shughuli za nyuklia za Iran kamwe hazijawahi kutoka kwenye mkondo wake wa kisheria.

Sasa hivi washauri wa rais mpya wa Marekani wanajaribu kukwepa ahadi zao na wanataka kuibebesha Tehran makubaliano mapya yasiyo ya JCPOA. Hata hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mara chungu nzima imetangaza wazi kwamba, mapatano yatakuwa ni hayo hayo ya nyuklia ya JCPOA. Uwezo wake wa kiulinzi na makombora ni mstari mwekundu kwake na kamwe Marekani haiwezi kulitwisha taifa la Iran mazungumzo mapya yaliyoko nje ya makubaliano ya JCPOA.

Tags