Jan 22, 2021 02:31 UTC
  • Iran yakaribisha wito wa kufanyika mazungumzo kwa ajili ya kuleta amani na maelewano katika eneo

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku zote imekuwa ikisisitiza udharura wa kufanyika mazungumzo na kuheshimiana mataifa ya eneo la Asia Magharibi na hasa Ghuba ya Uajemi na kutangaza wazi hamu yake ya kutaka kuwa na uhusiano mzuri na wa kimantiki na majirani zake wote.

Akizungumzia suala hilo Jumanne usiku, Muhammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu alisisitiza tena jambo hilo kupitia ujumbe wa Twitter na kukaribisha pendekezo lililotolewa na Waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Qatar la kutaka kuwepo mazungumzo kati ya Iran na nchi za Kiarabu za kusini mwa Ghuba ya Uajemi.

Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar alisema kuwa nchi yake iko tayari kuwa mpatanishi kwa ajili ya kufanyika kikao baina ya nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kabla ya hapo Iran tayari ilikuwa imezitaka nchi za eneo kushiriki katika mazungumzo na kujiunga na muungano wa kieneo kwa ajili ya amani.

Akizungumza katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2019, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alizitaka nchi zote ambazo zinazohusika na masuala ya Ghuba ya Uajemi na lango la Hormoz, kujiunga na 'muungano wa matumaini' yaani 'Ubunifu wa Amani ya Hormoz'

Muungano huo umejengeka katika misingi kadhaa muhimu kama vile kuheshimiwa tawala na ardhi za mataifa, kutatuliwa kwa amani hitilafu zote na kufungamana na misingi miwili muhimu ya 'kutochokoza' na 'kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine.'

Muhammad Javad Zarif

Ujumbe wa Twitter wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran bila shaka unathibitisha kwa mara nyingine kwamba Iran inalipa umuhimu mkubwa suala la nchi za eneo kujidhaminia zenyewe usalama wao wa Ghuba ya Uajemi.

Abdallah bin Swaleh Ba'boud, mtafiti wa uhusiano wa kimataifa anasema kuhusus suala hilo kwamba: Mazungumzo na ushirikiano wa Iran na nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi unaweza kuleta amani na uthabiti katika eneo na hivyo kupunguza kwa kiwango kikubwa uwepo wa wageni na mashindano ya silaha katika eneo.

Ni wazi kuwa kulinda usalama wa eneo hakuhitajii uwepo wa wageni wala mashindano makubwa ya silaha. Bila shaka fikra ya ushirikiano katika hatima ya pamoja ni suala linalohitajia nia njema na kujiepusha na tuhuma na madai yasiyo na msingi.

Marekani na utawala haramu wa Israel zimekuwa zikitumia suala la eti 'tishio la Iran' kama chombo cha kuibua migogoro katika eneo. Siasa hizo mbovu na haribifu ziimevruga kabisa usalama na utulivu wa eneo na wakati huo huo kueneza ugaidi wa Daesh katika eneo hili muhimu na la kistratijia. Pamoja na hayo urundikaji wa majeshi ya Marekani katika eneo na hata katika nchi za Afghanista na Iraq haujasaidia lolote katika kudhamini usalama wa maeneo hayo. Hili linatokana na ukweli kwamba hakuna wakati ambao nchi hiyo ya Magharibi imetaka kudhamini usalama wala kupambana na ugaidi katika maeneo hayo. Katika kipindi chote cha utawala wake, Trump huku akiwataja watawala wa nchi za Kiarabu kuwa ni 'ng'ombe wa maziwa' amewadaa kuamini kwamba Iran ni 'tishio' na hivyo kuandaa uwanja wa kuwauzia silaha ili kuepusha kufilisika makampuni ya Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliandika katika ukurasa wake wa Twitter mnamo tarehe 8 Disemba akisema: Majirani wapendwa! Ni kwa nini mnataka Marekani na nchi tatu za Ulaya zishiriki kwenye mazungumzo yenu na Iran? Hii ni katika hali ambayo, kwanza hakuna mazungumzo yoyote yatakayofanyika na nchi hizo kuhusu eneo hili kwa sababu zenyewe ni sehemu ya matatizo ya eneo hili. Pili, tunaweza kuzungumza moja kwa moja bila ya uingiliaji wa wageni. Ubunifu wa Amani ya Hormoz bado upo mezani.

Askari wa Marekani katika Ghuba ya Uajemi

Maneno na maandishi haya yanasisitiza ukweli kwamba Iran daima imekuwa ikikaribisha mazungumzo na majirani zake. Mipango kama vile Usalama wa Eneo wa 1986 na Jukwa la Mazungumzo ya Eneo la 2016, ni mipango inayothibitisha nia hiyo njema ya Iran, ambapo kwa sasa eneo hili linahitajia zaidi mipango kama hiyo kuliko wakati mwingine wowote.

Hatua ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kukaribisha mapendekezo ya mazungumzo ya amani inatokana na msingi madhubuti wa kuzingatiwa mitazamo ya pande kadhaa na kuamini uwezo wa nchi za eneo katika kutekeleza majukumu ya pamoja na kutembea katika njia moja ya kuleta amani na usalama wa kudumu kwa manufaa ya wote.