Jan 22, 2021 08:20 UTC
  • Catherine Ashton: Baada ya Iran kupata ushindi dhidi ya Trump, haitasalimu amri

Catherine Ashton, Mkuu wa zamani wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema katika makala ya pamoja na Chuch Hagel, Waziri wa Zamani wa Ulinzi wa Marekani kwamba, Washington inapaswa kurejea katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Katika makala yao hiyo, Ashton na Hagel wamepinga vikali hoja zinazotolewa za kupinga kurejea Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ambapo wahusika wanaamini kuwa, hali ya ulimwengu kwa sasa imebadilika ikilinganishwa na mwaka 2015 kulipofikiwa makubaliano hayo. 
Catherine Ashton na Chuck Hagel kadhalika wamebainisha kuwa, baada ya Jamhuri ya Kiislamu kushinda mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa yaliyokuwa yakitekelezwa dhidi ya Tehran na serikali ya zamani ya Marekani chini ya uongozi wa Donald Trump, taifa hili halitasilimu amri.
Maafisa hao wa zamani wa Umoja wa Ulaya na Marekani wamemtaka Rais mpya wa Marekani Joe Biden airejeshe Washington katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

 

Aidha wamesema kuwa, hatua yoyote ile ya kulazimisha kuweko mazungumzo mapya ni jambo ambalo halitakuwa na natija nyingine ghairi ya kushindwa na kugonga ukuta.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, katika siku za hivi karibuni viongozi wa Russia na China wamekuwa wakiitaka Marekani irejee katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA bila masharti.

Tarehe 8 Mei 2018, Marekani ilijitoa kijeuri katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia yanayojulikana kwa jina maarufu la JCPOA, lakini baadaye ikaanza kufanya njama kubwa za kujaribu kuzuia utekelezaji wa makubaliano hayo hasa kipengee cha kuondolewa Iran vikwazo vya silaha kwa mujibu wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, njama ambazo nazo zilifeli.