Jan 23, 2021 11:49 UTC
  • Zarif: Mlango wa fursa kwa utawala mpya wa Marekani hautabaki wazi milele

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemuasa Rais mpya wa Marekani Joe Biden, ahitimishe sera za mashinikizo zilizogonga mwamba za mtangulizi wake Donald Trump na kusisitiza kuwa, "dirisha la fursa kwa timu mpya ya Ikulu ya White House halitabakia wazi milele."

Mohammad Javad Zarif amesema hayo katika makala iliyochapishwa jana Ijumaa na jarida la Marekani la Foreign Affairs na kuelekeza bayana kuwa, aliyekuwa Rais wa Marekani, Donald Trump alishindwa kulifanya taifa la Iran lisalimu amri kwa kampeni yake ya mashinikizo ya juu kabisa. Amemtaka Biden aanzishe mchakato wa kuirejesha Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ya mwaka 2015 sambamba na kuiondolea nchi hii pasi na masharti yoyote vikwazo vya upande mmoja vilivyowekwa na utawala wa Trump.

Dakta Zarif amesema kutokana na mashinikizo ya Marekani, nchi za Ulaya zilizosaini mapatano hayo ya nyuklia zimeshindwa kutekeleza majukumu yao, hatua iliyoilazimisha Tehran kujibu mapigo, kwa kupunguza uwajibikaji wake katika mapatano hayo, kwa kutumia kipengee cha 36 cha JCPOA.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa, sera ya mashinikizo ya Trump iliwasababishia wananchi wa Iran uzito kwa kiasi fulani, lakini changamoto hizo hazikuwafanya waipigie magoti serikali ya Washington.

Trump (kulia) na Joe Biden

Zarif amesisitiza kuwa: Utawala mpya wa Washington una chaguo muhimu la kukhitari; ama ukumbatie sera zilizofeli za utawala wa Trump na uendelee kukanyaga sheria za kimataifa, au uachane na yaliyopita na ufungue ukurasa mpya wa kuimarisha amani na ushirikiano wa pande kadhaa katika eneo. 

Amesema iwapo Biden ataamua kukhitari chaguo sahihi la kuirejesha Marekani katika JCPOA na kuliondolea taifa hili vikwazo haramu, basi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia itarejea katika mkondo wa kutekeleza kikamilifu wajibu wake katika mapatano hayo ya kimataifa.

 

Tags