Jan 23, 2021 12:12 UTC
  • Rouhani: Iran kuanza kutoa chanjo ya Covid-19 ndani ya siku chache zijazo

Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itaanza kutoa chanjo ya kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 hapa nchini katika kipindi cha siku chache zijazo.

Rais Rouhani amesema hayo leo Jumamosi katika makao makuu ya jopokazi la kukabiliana na janga la corona hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, taifa hili linajitahidi lianze kampeni ya nchi nzima ya kutoa chanjo ya kupambana na corona kabla ya kumalizika mwezi huu wa Kiirani wa Bahman unaoisha Februari 18.

Dakta Rouhani ameeleza bayana kuwa,  katika mwaka ujao wa Kiirani wa 1400 (kuanzia Machi 21, 2021), Jamhuri ya Kiislamu itakuwa imezalisha aina tatu za chanjo ya corona.

Chanjo ya corona inayojulikana kama COVIRAN Barakat ambayo imetengenezwa na watafiti Wairani ilianza kufanyiwa majaribio kwa wanadamu Disemba 29 mwaka uliomalizika, ambapo idadi kubwa ya watu walijitolea kushiriki majaribio hayo.

Hadi sasa watu wote waliodungwa chanjo hiyo hawajapata madhara au taathira hasi za kiafya, na hivyo inatarajiwa kuwa chanjo hiyo itazalishwa kwa wingi katika siku zijazo na kutumika hapa Iran na maeneo mengine duniani. 

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya ya Iran, idadi ya watu waliogunduliwa kupatwa na ugonjwa wa Covid-19 nchini Iran hadi hivi sasa imefikia 1,367,032, ambapo 1,158,475 miongoni mwao wamepata afueni.

Watu 69 wameaga dunia kwa ugonjwa huo ndani ya saa 24 zilizopita, na kupelekea idadi jumla ya watu waliofariki dunia hadi sasa humu nchini kutokana na ugonjwa huo kufikia 57,294.

Tags