Jan 24, 2021 02:31 UTC
  • Twitter ya Zarif kwa Biden; chaguo la msingi la imma kuendeleza siasa zilizofeli au kurejea katika njia ya amani na utulivu

Makosa makubwa zaidi katika mahesabu ya sera za nje za Marekani yamejiri wakati wa utawala wa rais wa zamani wa nchi hiyo Donad Trump.

Trump alishadidisha siasa za uchupaji mipaka kimataifa na kuiwekea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vikwazo vikali mno, kwa ndoto za kulipigisha magoti taifa kubwa la Kiislamu la Iran; hata hivyo ndoto yake haikuaguka, na ameondoka madarakani kwa madhila akiicha Jamhuri ya Kiislamu ikizidi kuwa imara. Trump alifanya njama kubwa sana za kujaribu kusambaratisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA, aliweka mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa ya kiuchumi kupitia vikwazo, alifanya njama za kuvutia uungaji mkono wa kimataifa na alitaka dunia iirejeshee Iran vikwazo vya silaha vya Baraza la Usalama, lakini kote huko amegonga mwamba. Kosa kubwa la Trump ni kwamba hakuwahi kufikiria kuwa Iran itaweza kusimama imara na kukabiliana na mashinikizo yote hayo ya Marekani na ni dhahir shahir kuwa rais huyo wa zamani wa Marekani alifanya makosa ya kimahesabu.  

Mapatano ya nyuklia ya JCPOA yaliyopasishwa na Baraza la Usalamam la UN 

Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran juzi Ijumaa aliashiria katika ukurasa wake wa Twitter namna serikali mpya ya Marekani ilivyo na chaguo la msingi mbele yake na kuandika: serikali ya Biden inaweza kuendeleza siasa hizo zilizofeli za huko nyuma au kuendelea na njia ya kukandamiza ushirikiano na sheria za kimataifa au  kupinga na kuachana na dhana zilizofeli na badala yake ifuate njia ya amani na utulivu. 

Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran  

Maamuzi yasiyo ya kiadilifu na makosa makubwa yaliyofanywa na Trump miaka minne iliyopita si tu yamekosolewa pakubwa kimataifa bali yamechafua pia taswira ya Marekani duniani.  

Vadim Khomenkov, Mhadhiri wa Chuo Kikuu na Naibu wa Akademia ya Sayansi ya Jamhuri ya Tatarstan huko Russia anaamini kuwa: kujitoa kwa upande mmoja Marekani katika mapatano ya JCPOA pia lilikuwa kosa la kiistratejia la Donald Trump ambalo limeitia hasara kubwa Marekani na kuiondolea itibari duniani.   

Hatua zilizochukuliwa na Iran kwa ajili ya kupunguza uwajibikaji wake wa khiari katika fremu ya mapatano ya JCPOA zimeidhihirishia Marekani uhakika kwamba Tehran katu hainyamazi kimya mbele ya lugha za vitisho na mabavu za watawala wa White House.    

Katika sehemu moja ya hotuba yake ya hivi karibuni kwa mnasaba wa maadhimisho ya kumbukumbu ya mapambano ya wananchi wa mji wa Qum ya tarehe 19 mwezi Dei mwaka 1356 Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliashiria suala la JCPOA na kueleza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina haraka wala haitilii mkazo kivyovyote kurejea Marekani katika mapatano ya JCPOA bali takwa letu la kimantiki ni kuondolewa vikwazo na mataifa mbalimbali kurejeshewa haki zao zilizoghusubiwa ambalo ni jukumu la Marekani na waitifaki wake.  

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu 

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja uamuzi wa serikali ya Iran wa kupunguza sehemu nyingine ya ahadi zake za hiari ndani ya mapatano ya JCPOA kuwa ni uamuzi sahihi kikamilifu na ni wa busara na kuongeza kuwa: Itakuwa ni upuuzi kama Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kutimiza majukumu yake yote peke yake tu katika hali ambayo upande wa pili haujali majukumu yake. Iwapo wao watarejea katika majukumu yao sisi pia tutarejea.  

Ukweli wa mambo ni kuwa uadui wa Marekani kwa Iran unasababishwa na nchi hii kutokubali siasa za ukandamizaji na dhulma za Marekani; kwa hivyo njia pekee ya kukomesha uadui huo ni kuwakatisha tamaa maadui na ndio maana tunapasa kuwa imara na kuimarisha nyenzo halisi za nguvu yetu. Matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia yanabainisha wazi msimamo wa kimantiki wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu mapatano ya JCPOA. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran juzi Ijumaa pia aliashiria katika makala iliyochapishwa kwenye jarida la Foreign Affairs kuhusu siasa zilizofeli za serikali ya Trump na kueleza kuwa; serikali mpya ya Biden iliyoingia madarakani ingali inaweza kuyanusuru mapatano hayo ya nyuklia lakini kwa sharti kwamba vikwazo vyote vilivyowekwa, vilivyorejeshwa tena na kuhuishwa upya tangu Trump aingie madarakani dhidi ya Iran, viondolewe.