Jan 24, 2021 14:01 UTC
  • Waziri wa Afya wa Iran: Utoaji chanjo ya corona nchini utaanza hivi karibuni

Waziri wa Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran amesema, utoaji chanjo ya corona hapa nchini utaanza hivi karibuni.

Kwa mujibu wa IRIB, Saeed Namaki ameeleza hayo leo alipoashiria juhudi zilizofanywa ili kutengeneza chanjo ya corona inayotokana na wataalamu wa humu nchini na akaongeza kuwa, uingizaji chanjo ya corona iliyotengenezwa nje ya nchi pia utaanza hivi karibuni.

Namaki amesema, baada ya kuingizwa chanjo ya corona kutoka nje ya nchi, utoaji wa chanjo hiyo utaanza kwa kuhusisha makundi ya watu wenye hali hasasi kiafya na walioko kwenye mazingira hatarishi zaidi.

Wauguzi wa wagonjwa wa corona Iran

Wakati huohuo, Hojjatollah Niki Maleki, mkuu wa kitengo cha habari cha tume ya utekelezaji maagizo ya Imam Khomeini (MA) amesema, baada ya kuchunguzwa hali za watu 21 waliojitolea kupigwa chanjo ya corona iliyotengenezwa nchini , kibali kingine kimetolewa cha kuruhusu kuwadunga chanjo hiyo watu wengine 14 waliojitokeza wenyewe kupatiwa chanjo hiyo kwa ajili ya majaribio.

Awamu ya kwanza ya kuifanyia majaribio kwa binadamu chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 iitwayo COVIRAN Barakat ambayo imetengenezwa na wanasayansi wa Kiirani ilianza kutekelezwa tarehe 29 Desemba 2020.../

Tags